SERIKALI ya Marekani, imepiga marufuku ya usafiri dhidi ya raia wa Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa ya Ikulu ya Marekani, iliyotolewa leo Jumatano, tarehe 17 Desemba 2025, imeeleza kuwa hivi ni vikwazo vipya kwa taifa hili la Afrika Mashariki.
White House imesema, vikwazo hivyo vinavyokusudia “kulinda usalama wa Marekani,” na kwamba vitaanza kutumika kuanzia 1 Januari 2026.
Katika amri hiyo, iliyotiwa saini na Rais Donald Trump, Jumanne tarehe 16 Desemba, utawala wa Marekani umeijumuisha Tanzania katika orodha ya nchi zinazokabiliwa na vikwazo vya muda vya kuingia nchini humo.
Sababu iliyotolewa, ni uzembe wa ukaguzi, uhakiki na upashanaji habari wa mamlaka ya Tanzania kuhusu raia wao.
Oktoba mwaka huu, Serikali ilisema, imeanza mashauriano rasmi na Serikali ya Marekani kuhusu masuala ya uhamiaji ambayo ilihofia inaweza kuathiri uwezo wa raia wake kuingia nchini humo.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alinukuliwa akisema, mashauriano kati ya Tanzania na Marekani, yanafanyika kupitia wizara ya mambo ya nje.
Mashauriano hayo ya masuala ya kibalozi pamoja na mambo mengine yanagusa utoaji wa nyaraka halali za utambulisho na kushirikiana katika masuala ya uhamiaji.
Hatua ya Marekani kuiwekea vikwazo Tanzania, inakuja takribani siku 45, tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, uliotajwa na waangalizi wa kimataifa kuwa “haukuwa huru na haki.”
Aidha, uchaguzi mkuu wa Tanzania wa 29 Oktoba, ulikumbwa na maandamo yenye ghasia, vifo kwa waandamanaji na wasiokuwa kwenye maandamano na raia wengine kadhaa kujeruhiwa.
Vyombo vya habari vya kimataifa, vimeripoti kuwa zaidi ya watu 7,000 wamefariki dunia, huku upinzani ukidai kuwa zaidi ya watu milioni moja waliuawa wakati na baada ya uchaguzi huo.

Mpaka sasa, Serikali haijatoa idadi kamili ya waliofariki dunia na haijaeleza iliiko miili ya waliofikwa na mauti.
Nchi nyingine za Afrika zinazokabiliwa na vikwazo hivyo ni Burkina Faso, Mali, Niger, Sudan Kusini, Syria pamoja na watu walio na pasipoti ya Mamlaka ya Palestina.
Laos na Sierra Leone, ambazo hapo awali ziliwekewa vikwazo vya muda, sasa zimejumuishwa kwenye orodha ya nchi 15 zilizopigwa marufuku, ikiwa ni pamoja na Nigeria, Tanzania na Zimbabwe.
Serikali ya Trump imesema, imechukua hatua hiyo kutokana na kile ilichokitaja kuwa viwango vya juu vya visa vya watu ambao wanasalia nchini mwake kwa muda mrefu baada ya muda wao kuisha kwa jambo la msingi.
Wakati wa muhula wake wa kwanza, alianzisha agizo kama hilo mnamo 2017, ambalo lilizua maandamano na changamoto za kisheria ndani na nje ya nchi. Sera hiyo baadaye ilizingatiwa na Mahakama ya Juu ya Marekani.
Marekani imesema, vikwazo vitaendelea kuudumishwa hadi nchi zilizoathirika zifanye “maboresho ya kuaminika.”
ZINAZOFANANA
Makamu wa Rais aongoza mazishi ya Jenista Mhagama
Utawala wa sheria ndani ya kiza kinene
Mwambe, IJP, Muliro kuumana mahakamani leo