December 17, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kamati ya maboresho ya TASWA yakamilisha jukumu lake

Mwenyekiti wa TASWA, Amir Mhando

 

KAMATI Maalumu iliyoundwa kwa ajili ya Kuandaa Mabadiliko ya Mfumo wa Uendeshaji wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) imekamilisha jukumu hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mwenyekiti wa TASWA, Amir Mhando, amesema kamati hiyo inayoongozwa na Mhariri mkongwe nchini, Joseph Kulangwa, imeandaa ripoti hiyo kwa kushirikiana na taasisi ya Frux, iliyopewa jukumu la kuwa Mshauri Mwelekezi na Kamati ya Utendaji ya TASWA kuandaa Mpango Mkakati na kukifanya chama kijiendeshe kisasa zaidi kulingana na mabadiliko ya wakati.

Kwa mujibu wa Mhando, Wajumbe wa kamati hiyo ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Egbert Mkoko, Mkurugenzi wa Utafiti na Machapisho wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dar es Salaam, Dk. Dominic Nkolimwa, Mhariri Mtendaji wa UTV, Frank Sanga, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), William Shao, Katibu Mkuu mstaafu wa TASWA, Abdul Mohammed na CPA Shija Richard, ambaye amepata kwa Mhazini wa TASWA na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Tunaishukuru Kamati pamoja na Frux kuandaa Ripoti ya Mpango Mkakati wa chama kwa miaka mitano ( 2026-2031), hiyo ni hatua kubwa kuelekea TASWA mpya tunayoitamani wote.

“Kamati ya Utendaji ya TASWA itakutana wiki hii kuandaa mkutano wa wadau wote muhimu kuzindua Mpango Mkakati huo na kuanza rasmi utekelezaji wake.

“Hata hivyo mapendekezo mengine ya mabadiliko ya kimfumo yameingizwa kwenye rasimu ya mabadiliko ya Katiba ya chama kama ilivyoshauriwa na kamati na yatapelekwa kwa wanachama kwa ajili ya hatua nyingine,” amesema Mhando.

About The Author

error: Content is protected !!