MATUKIO ya wananchi kutekwa, kuteswa na kutoweka yanayodaiwa kufanywa na serikali na “watu wasiojulikana,” yanazidi kuiweka njiapanda serikali. Anaandika Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Serikali ndiyo yenye jukumu la kikatiba na kisheria la kulinda raia na mali zao. Hatua ya serikali kushindwa au kutekeleza kutekeleza wajibu huo, ni doa kubwa kwa walioko madarakani.
Matukio ya wananchi kutekwa, kuteswa, kuuawa na kukamatwa kiholela, yamekuwa yakiripotiwa kwa wingi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Kwa mfano, Agosti mwaka jana, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deusdedith Soka na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise, walidaiwa kutekwa na mpaka sasa, bado hawajapatikana.
Jeshi la polisi na vyombo vingine vya usalama nchini, havijaeleza uchunguzi wa suala hilo umefikia wapi. Hawajaeleza nani anayeshikiliwa na hata kuhisiwa kufanya kitendo hicho.
Soka na wenzake jijini Dar es Salaam. Kabla ya kutoweka waliripoti kupokea wito wa polisi kwa njia ya simu, ukiwataka kufika kituo cha polisi Chang’ombe, ili kuchukua pikipiki yao, iliyokuwa inashikiliwa.
Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, iliamuru jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kubaini mahali aliko Soka na wenzake.

Ni mwaka mmoja na ushei sasa, Soka, Mbise na Mlay, hajawapatikana na hakuna dalili ya kuwa bado wako hai.
Peter Madeleka, Wakili wa Mahakama Kuu, aliyemuwakilisha Soka na wenzake, alikwenda mahakamani na kuomba kutolewa amri kwa polisi kuwaleta waleta maombi mahakamani. Hakufanikiwa.
Mahakama ilikubaliana na hoja yake, lakini wakaagiza polisi kufanya uchunguzi wa suala hilo, bila kutoa muda wa uchunguzi huo.
“Kwa njia hizi za kimahakama, hakuna namna yoyote ya mahakama kuingilia katia kulinda maisha na uhai wa watu. Mhimili wa mahakama umeingiliwa na mhimili wa serikali na hivyo, wananchi waliowengi wamepoteza matumaini ya kupata haki,” anaeleza.
Edgar Mwakabela ‘Sativa,’ naye ni miongoni mwa watu walioripotiwa kutekwa mwaka 2024.
Sativa akitekwa tarehe 23 Juni 2024 na kupatikana tarehe 27 Juni katika Pori la Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha mwilini.

Humphrey Polepole, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, naye ametekwa na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika.”
Familia yake, walitangaza kuwa Polepola alitekwa kutoka nyumbani kwake, Ununio jijini Dar es Salaam, usiku wa tarehe 6 Oktoba 2025.
Polisi walidai kuanza uchunguzi. Familia ikafungua shauri mahakamani, kupigania ufichuzi wa mahali alipo. Mpaka sasa, hajaweza kupatikana na mahakama haikusaidia kujua mahali aliko.
Kabla ya kukutwa na dhahama hiyo, Polepole alimwaga tuhuma kadhaa dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wake. Alidai kuwa chama hicho, kimetekwa na wanamtandao na kimekumbatia ufisadi na mafisadi.
Alimtuhumu binafsi mwenyekiti wake, Samia Suluhu Hassan, kujipitisha kuwa mgombea urais, kinyume na katiba, kanuni na taratibu za chama chao.
Matamshi ya Polepole yalikuwa mwiba mkali kwa watawala, kutokana na nyadhifa alizowahi kushika serikkalini na kwenye chama.

Polepole ameshika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, taifa; mkuu wa wilaya, mbunge na balozi.
matukio haya yamezua mijadala mikubwa nchini. Wapo wanaosema, hata maandamano ya 29 Oktoba, yalichochewa na kushamiri kwa vitendo hivyo.
“Ni kweli, wale waandamanaji, pamoja na mambo mengine, walidai kukomeshwa kwa vitendo vya utekaji, utesaji na mauaji. Walikuwa wanadai kuwapo kwa utawala wa sheria, haki ya kuishi na uhuru wa mawazo,” anaeleza Joseph Selasini, aliyekuwa mbunge wa Rombo (Chadema).
Jitu Omari, mkazi wa Dar es Salaam alisema, kuwepo kwa magenge ya utekaji nchini, kunatishia usalama wa raia. Anasema, “hebu fikiria watekaji wananguvu kuliko polisi. Wanateka na mtu anayetekwa hapatikani na maisha yanaendelea.”
Mdude Nyagali kada maarufu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alivamiwa na kutekwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake usiku wa terehe 2 Mei mwaka 2025 .
Jeshi la polisi mkoani Mbeya lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa inaendelea na uchunguzi lakini mpaka leo hakuna matokeo yoyote ya uchunguzi huo na Mdude hajapatikana.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, amesema matendo ya utekaji yameshamiri nchini na kuitaka serikali kuyakabili magenge hayo, iwapo kweli hawahusiki nayo.
Anasema, “Kuna matukio mengi ya watu kutekwa na kupotezwa. Wengi waliokumbwa na mambo haya, ni wanaharakati, waandishi wa habari na wanasiasa wanaopinga au kuikosoa serikali.”
Anaongeza, “matukio haya, yanahusishwa moja kwa moja na vyombo vya dola. Ni matukio yanayokuja kwa malengo ya kutia hofu wananchi wasiendelee kudai wanachoamini kuwa ni haki yao.”
Anasema, serikali imeridhia mikataba ya kimataifa na hivyo, ni muhimu kuitekeleza kwa vitendo.
“Tunaomba viongozi wetu kuridhia mkataba wa kimataifa kuhusu ulinzi wa watu wote dhidi ya utekaji na upoteaji wa kulazimishwa. Ndani ya mikataba hiyo, kuna sheria inayosimamia na kukataa utesaji na vitendo vya utekaji,” anaeleza.
Mwanahakati wa haki za binadamu, Godlisten Malisa, amedai matukio ya watu kupotea na kutekwa yameanza kurejea akimaanisha yalififia.

“Kwa siku za hivi karibuni matukio haya yameanza kurejea na kurudisha mashaka, wananchi wanataka kuona Serikali inakomeshaje matukio haya,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Malisa, Serikali inapaswa kuyachukulia matukio ya utekaji kwa uzito mkubwa, ikiwamo kuundwa kwa Tume ya Kijaji kuchunguza matukio hayo.
“Serikali iwachukulie wanaotoa taarifa za utekaji kama watu wema, sio kuwamakata, kwa sababu sio wahalifu bali itoe ushirikiano,” amesema Malisa.
Septemba mwaka jana, Mjumbe wa Sektarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ally Mohamed Kibao, alishushwa kwenye basi la Tashrif, maeneo ya Tegeta. Alikuwa akirejea nyumbani kwake, mkoani Tanga.
Kada wa Chadema, alishushwa kwenye gari na watu wenye silaha, ambao mpaka leo hawajatajwa.
Tume iliyoundwa na Rais, haijaweka wazi ripoti yake, badala yake, mkuu huyo wa nchi alisema, “kifo cha mtu mmoja tu, watu wanapiga kelele zote hizo?”
Matukio haya yanaiondolea Tanzania sifa kuwa nchi yenye utawala wa sheria kwa kuwa utawala wa sheria umetafsiriwa kwenye muktadha wa mambo matano:
Kuheshimu na kulinda haki za binaadamu, vyombo vya dola kufanya kazi kwa mujibu wa sheria; uwajibikaji, uwazi na mahakama kuwa huru.
Utawala wa sasa nchini, umeshindwa kuzingatia misingi ya utawala bora. Hauzingatii maoni na ridhaa ya walio wengi.
ZINAZOFANANA
Mwambe, IJP, Muliro kuumana mahakamani leo
Jiji kubwa, changamoto kubwa: Uhaba wa maji waitesa Dar
Uhusiano na ACT-Wazalendo, bado uko imara – Mpina