MAKAMU wa Rais wa Tanzania Emmanuel Nchimbi amewaongoza waombolezaji kwenye Mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Marehemu Jenista Mhagama, yaliyofanyika katika Kijiji cha Ruanda Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma leo tarehe 16 Desemba 2025. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Akitoa salamu za rambirambi mara baada ya mazishi hayo, Makamu wa Rais amesema marehemu Jenista Mhagama alikuwa mtumishi wa kweli wa watu wake ambaye aliwatumikia na kuwajali,Pia amesema kama serikali wamepoteza mtu muhimu ambaye mchango wake hautasauhaulika katika nyadhifa mbalimbali ambazo amewahi kutumika.
Nchimbi ameongeza kwamba Serikali na Chama Cha Mapinduzi itaendelea kuenzi mchango wa marehemu Jenista Mhagama kwa kuendelea kuwa watetezi wa wananchi wa chini, ambapo ametoa wito kwa Viongozi wa Serikali kuhakikisha wananchi wa hali ya chini ndio wanakuwa kipaumbele chao cha kila siku.

Aidha Makamu wa Rais amewasilisha salamu za shukrani za Rais wa Tanzania Samia Hassan alizozitoa kwa familia na wananchi wa Ruvuma kwa ujumla kutokana na maisha ya marehemu Jenista Mhagama.
Pia amewashukuru Viongozi wa Kanisa ambao wameshiriki katika Ibada mbalimbali zilizofanyika za kumuombea marehemu Jenista Mhagama kuanzia mkoani Dodoma hadi mkoani Ruvuma.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kumsimamia vema mkandarasi anayejenga barabara ya Kitai hadi Ruanda ili aweze kuendana na kasi iliyotarajiwa. Amesema tayari Serikali ilikwisha kutoa fedha za za ujenzi wa barabara hiyo kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo katika uchumi.
Spika wa Bunge la Tanzania Mussa Zungu ameishukuru Serikali,Bunge, Mawaziri, Wabunge, familia na wananchi wote kwa kujitoa na kuhakikisha Marehemu Jenista Mhagama anapumzishwa kwa heshima na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani.
ZINAZOFANANA
Utawala wa sheria ndani ya kiza kinene
Mwambe, IJP, Muliro kuumana mahakamani leo
Jiji kubwa, changamoto kubwa: Uhaba wa maji waitesa Dar