MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu, tarehe 15 Desemba 2025, inatarajiwa kusikiliza kesi iliyofunguliwa na Geoffrey Mwambe, waziri wa zamani katika serikali ya John Magufuli na Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Masasi, mkoani Mtwara. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mwambe amefungua mashitaka mahakamani, kupinga hatua ya mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP), mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP), na mkuu wa upelelezi kanda maalum ya Dar es Salaam (ZCO DSM), kumshikilia kinyume na sheria.
Kesi hiyo, yenye Na 289778/2025, imefunguliwa mahakamani hapo na Mwambe, kupitia wakili wake, Hekima Mwasipu.
Kwa mujibu wa rekodi za mahakama, maombi hayo, yanatarajiwa kusikilizwa mbele ya Hakim Mkazi, Gwantwa Mwankuga.
Mwambe alikamatwa wiki iliyopita na amekuwa akishikiliwa na jeshi la polisi kwa kile wanachoita, “kujihusisha na makosa ya jinai.”
Taarifa ya jeshi hilo, iliyotolewa tarehe 12 Desemba mwaka huu na Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ilieleza kuwa “Mwambe anashikiliwa kwa tuhuma za jinai ambazo zinachunguzwa.”
Katika taarifa hiyo, jeshi hili limesema, lilimkamata Mwambe, usiku wa tarehe 7 Desemba 2025, nyumbani kwake, huko Tegeta, wilayani Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, huku likieleza kuwa hatua kali za kisheria dhidi yake zinakamilishwa.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa mmoja wa wanafamilia wa mwanasiasa huyo anasema, jeshi la Polisi limemhoji Mwambe kwa mambo kadhaa, ikiwamo uhusiano wake na mmoja wa viongozi wajuu wa serikali.
Aidha, aliyekuwa mbunge wa Masasi mkoani Mtwara (CCM), katika Bunge lililopita, anadaiwa kupokea kipigo kizito, ili aweze kutaja uhusiano wake na kiongozi huyo na wanachozungumza wanapokutana.
ZINAZOFANANA
Jiji kubwa, changamoto kubwa: Uhaba wa maji waitesa Dar
Uhusiano na ACT-Wazalendo, bado uko imara – Mpina
Rais Samia aongoza waombolezaji ibada ya mazishi ya Jenesta