WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) imesaini mikataba ya kufunga miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwa shule za Sekondari 52 na Chuo cha VETA kimoja hapa nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hafla hiyo ya utiaji saini imeongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy hii leo tarehe 4 Desemba 2025 Jijini Dar es Salaam pamoja na Wawakilishi wa kampuni ya TAIFA Gas Ltd na Hanny G Ltd ikiwa ni sehemu ya awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mkataba wa kuziwezesha Taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kufungiwa miundombinu ya nishati safi ya kupikia.
Saidy amesema, mradi huo utahusisha upelekaji wa mifumo ya nishati safi ya kupikia kwenye shule 52 za Sekondari na Chuo kimoja cha VETA ili kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi hapa nchini.
Ameongeza kuwa, mradi huo utanufaisha Walimu 2,192, Wanafunzi 54,405 na utatekelezwa katika mikoa 18 hapa nchini,pia mradi huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali kupitia REA ambazo zinalenga katika kuziwezesha Taasisi mbalimbali kutumia nishati safi ya kupikia.
Naye, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Advera Mwijage amesema gharama ya mradi huo ni shilingi bilioni 5.8 na wanufaika ni shule 52 za Sekondari na Chuo kimoja cha VETA.
“Mifumo itakayofungwa ni LPG ya kuanzia tani moja hadi mbili, masufuria ya kupikia yanayotumia LPG yenye mita za ujazo 50 hadi 300 masufuria ya kupikia yenye mita za ujazo 50 hadi 300 yanayotumia mkaa mbadala, pamoja na ununuzi wa mkaa mbadala wa kuanzia kwa Taasisi zote zinazonufaika,” Amesema Mwijage.
Aidha Mwijage ameeleza kuwa, Wakala ulishafunga mifumo katika shule mbili zilizopo Simiyu pamoja na Ruvuma. Ameongeza kuwa ufungaji wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika shule ya sekondari Ruhinda iliyopo katika mkoa wa Kagera unaendelea.
Kwa upande wake, Meneja wa Mauzo wa Taifa Gas, Mosses Massawe amemshukuru Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kuziwezesha Taasisi mbalimbali ili ziachane na nishati isiyo safi na salama na kuhamia katika matumizi ya nishati safi.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Hanny G Investment, Hanny Mbaria ameishukuru Serikali kupitia REA na kubainisha kuwa watatekeleza mkataba huo kikamilifu ili kuhakikisha Watanzania na Taasisi zinatumia nishati safi na salama.
ZINAZOFANANA
Meta yamjibu Mange Kimambi, yeye akimbilia kwa Trump
Umoja wa Mataifa, Marekani yaikaba koo Tanzania
Wanafunzi 937,581 wachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza, wasichana vinara