Umoja wa Ulaya
BALOZI 16 za nchi za magharibi zimetoa wito kwa Serikali ya Tanzania, kufanyika uchunguzi huru wa matukio ya 29 Oktoba; kuwaachia huru wanaozuiliwa na kukabidhi haraka miili ya waliouawa katika machafuko hayo. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Mabalozi wa Uingereza, Canada, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Denmark, Finland (Ufini), Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Poland, Slovakia, Hispania, Uswidi, pamoja na Umoja wa Ulaya (EU), wameeleza kusikitishwa na vitendo vya mauaji nje ya utaratibu wa kisheria, kupotea kwa watu, na ufichaji wa miili ya waliopoteza maisha.
Haya yanajiri siku tatu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kukiri kwamba ilikuwa sahihi kwa vyombo vya usalama, kutumia nguvu kukabiliana na waandamani aliyodai kuwa walilenga kupindua serikali yake.
Kwenye maandamano hayo ya siku tatu za uchaguzi, kuanzia tarehe 29 Oktoba hadi 3 Novemba, mamia ya watu wanaripoti kupoteza Maisha, kutokana na kushambuliwa na vyombo vya usalama.
Ripoti hizo zinajumuisha tuhuma za mauaji ya kiholela ya mamia ya watu, kutekwa nyara kwa nguvu, na kuwekwa kizuizini kiholela kwa maelfu hususan waandamanaji, viongozi wa upinzani na wanaharakati wa kiraia katika maeneo mbalimbali nchini.
Mabalozi walisisitiza kwamba Serikali ya Tanzania ina wajibu wa kutoa taarifa ya kina kuhusu hatima na mahali waliko watu wote waliotekwa nyara.

Mabalozi wanasema, “…ukamataji watu kiholela na ufichaji wa mili ya waliopoteza Maisha, haukubariki kwenye uso wa ulimwengu. Tunatoa wito kwa mamlaka husika kukabidhi mili ya marehemu kwa familia zao haraka iwezekanavyo, kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa na kuhakikisha waliokamatwa wanapata misaada ya kisheria na matibabu.”
Wameongeza, “Zaidi, tunatoa wito kwa serikali kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti za awali za waangalizi wa uchaguzi wa AU (Umoja wa Afrika) na SADC (Jumuya ya nchi zilizoko Kusini mwa Afrika), ambazo ziliweka bayana mapungufu yaliyojiri wakati wa mchakato wa uchaguzi.”
Aidha, mabalozi wameitaka serikali kuondoa mara moja vikwazo vyote vinavyokwamisha uhuru wa vyombo vya habari, wakisema vikwazo hivyo vinakiuka wajibu wa kimataifa chini ya mikataba ya haki za binadamu.
“Tunatambua azma ya serikali ya kudumisha amani na utulivu wa nchi, na tunasisitiza umuhimu wa vyombo vya ulinzi kutekeleza majukumu yao,” lakini wajibu huo, ni sharti uendane na wajibu wa kutenda haki kwa raia.
Balozi hizo zimeitaka Serikali pamoja na vyombo vya usalama kuhakikisha kulindwa kwa haki ya wananchi kukusanyika kwa amani, hasa kuelekea maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 9 Desemba 2025.
Walionya kuwa hatua yoyote itakayokiuka haki hiyo inaweza kuongeza mgogoro wa kibinadamu na kisiasa.
Hapo jana, Marekani ilisema, inatathimini upya uhusiano wake na Tanzania kufuatia mauaji ya raia wengi wakati wa uchaguzi huo.

Taarifa iliotolewa na ubalozi wa Marekani, ilisema kuwa licha ya uhusiano wake wa muda mrefu uliostawi kati yake na taifa hilo, hatua ya hivi karibuni ya taifa hilo imezua wasiwasi mkubwa kuhusu mwelekeo wa uhusiano huo.
Katika uchaguzi wa 29 Oktoba, viongozi wa vyama viwili vikuu vya upinzani nchini, walizuiwa au kuenguliwa kugombea, na wengine waliwekwa kizuizini au kupotezwa kabla ya siku ya kupiga kura.
Balozi hizo zimeitaka Serikali pamoja na vyombo vya usalama kuhakikisha kulindwa kwa haki ya wananchi kukusanyika kwa amani, hasa kuelekea maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 9 Desemba 2025.
Walionya kuwa hatua yoyote itakayokiuka haki hiyo inaweza kuongeza mgogoro wa kibinadamu na kisiasa.
Nao wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN), wamesema wako tayari kutoa msaada wa kiufundi kwa Serikali ya Tanzania ili kusaidia kurejesha mazingira ya kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

Akihutubia taifa kupitia wanaoitwa, “Wazee wa mkoa wa Dar es Salaam,” Rais Samia alitoa hotuba yenye uzito wa kisiasa ambayo imeibua mjadala mkali ndani na nje ya nchi.
Moja ya sehemu kali zaidi za hotuba hiyo ni pale Rais alipolenga mataifa ya nje, akisema yamekuwa yakitoa maagizo kuhusu jinsi Tanzania inavyopaswa kuendesha mambo yake. Alisema Tanzania haiwezi kukubali kudhibitiwa au kuwekewa masharti kwa kisingizio cha misaada au ushirikiano.
“Nje huko wanakaa ooh Tanzania ifanye hivi, ifanye vile… (wao kina nani) who are you? Wanadhani wao bado ni masters (watawala) wetu,” alihoji.
Kwa mujibu wake, Tanzania imekuwa ikilengwa kwa sababu ya utajiri wake wa kiasili, na iwapo wazawa hawatakuwa waangalifu, rasilimali hizo zinaweza kuwa chanzo cha migogoro ya kisiasa.
“Maumbile yetu na utajiri wetu isiwe laana tukauana sisi kwa sisi kwa kushawishiwa na wanaotolea macho nchi yetu,” alisema.
ZINAZOFANANA
Uwezekano wa wanawake kuwa Mashemasi bado mgumu
Meta yamjibu Mange Kimambi, yeye akimbilia kwa Trump
Umoja wa Mataifa, Marekani yaikaba koo Tanzania