WATAALAMU wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN), leo Alhamisi, tarehe 4 Desemba 2025, imetaka kuundwa kwa Tume mpya ya uchunguzi, kufuatia maandamano ya siku ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
“Serikali ya Tanzania lazima ianzishe uchunguzi wa haraka, usioegemea upande wowote, huru, wa kina, na wenye ufanisi kuhusu mauaji yote yaliyoripotiwa, kutoweka kwa watu kwa lazima, na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu,” imeeleza taarifa ya UN.
Kwa mujibu wa wataamu hao, kuanzishwa kwa tume ya uchunguzi kunalenga kuufahamisha umma na jumuiya ya kimataifa kuhusu sababu za maandamano na ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Tume mpya inapaswa kuwa huru na kutoa mapendekezo ya kuhakikisha uwajibikaji, haki na fidia, ikiwa ni pamoja na dhamana ya kutojirudia, na ushiriki kamili wa waathiriwa na mashirika ya kiraia,” wameeleza.
Umoja wa Matifa umesema, unalaani vikali ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini, na kwamba wanawasiliana na Serikali kuhusu suala hili na wako tayari kutoa msaada wa kiufundi kwa mamlaka za Tanzania, ili kufanikisha uchunguzi huo.

Miongoni mwa madai ya UN, ni pamoja na taarifa za mamia ya mauaji yasiyo ya haki, kutoweka kwa lazima na kuwekwa kizuizini kwa kiholela kwa waandamanaji, viongozi wa mashuhuri wa upinzani na asasi za kiraia.
“Serikali lazima itoe taarifa kuhusu hatima na mahali walipo watu wote waliotoweka na kuhakikisha utambuzi na urejeshaji wa mabaki kwa familia zao kwa heshima,” wataalamu walisema.
Wakaongeza, “vikwazo vyote vya uandishi wa habari lazima viondolewe, kwani haviendani na majukumu ya kimataifa ya Tanzania.”
Wataalamu hao walibainisha kuwa idadi ya watu waliouawa kinyume cha sheria baada ya uchaguzi inakadiriwa kuwa angalau watu 700, huku makadirio mengine yakionyesha maelfu ya waathiriwa.
Wamesema, kuna ripoti za kutisha kuhusu kutoweka kwa miili ya waathiriwa kutoka kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti, na madai kwamba mabaki ya watu yanachomwa au kuzikwa katika makaburi ya halaiki yasiyojulikana.
Wanasema, wanafamilia waliotambua mabaki waliripotiwa kulazimishwa kusaini taarifa za uongo kuhusu chanzo cha kifo, ili kuweza kupewa miili ya wapendwa wao.
UN inasema, uchaguzi uliendelea huku kukiwa na wasiwasi wa muda mrefu, ikiwa ni pamoja na kuwekwa kizuizini kiholela na kutoweka kwa lazima kwa watu mashuhuri wa upinzani, na mabadiliko ya kisheria ambayo yalidhoofisha haki ya mfumo wa uchaguzi.
Kwamba, viongozi kutoka vyama viwili vikuu vya upinzani walizuiliwa au hawakuruhusiwa kugombea, na katika baadhi ya visa walikamatwa au kutoweka kwa nguvu kabla ya uchaguzi.
Maandamano ya kupinga uchaguzi yalizuka kote nchini, hasa yakiongozwa na vijana, dhidi ya chama tawala cha siasa.
Jibu la Serikali lilidaiwa kuwa matumizi ya nguvu ya haraka na yenye kuua dhidi ya waandamanaji hawa na vikosi vya usalama, ikiwa ni pamoja na wanajeshi na polisi.

Wataalamu hao walisema kwamba ripoti za kusumbua zinaonyesha maafisa walipewa amri ya “kupiga risasi ili kuua” wakati wa amri ya kutotoka nje iliyotekelezwa.
Wataalamu hao walibainisha kuwa kufungwa kabisa kwa intaneti kulianzishwa kuanzia tarehe 29 Oktoba hadi 3 Novemba 2025, na kuzidisha mgogoro huo.
“Kuzimwa huku kulipunguza sana uwezo wa watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari kufanya kazi zao na kuandika ukiukwaji,” walisema.
Wakati hayo yakiendelea, serikali ya Marekani, leo tarehe 4 Desemba, imetangaza kupitia upya uhusiano wake na Tanzania huku kukiwa na wasiwasi kuhusu uhuru wa kidini, uhuru wa kujieleza, vikwazo kwa uwekezaji wa Marekani na vurugu dhidi ya raia.
Marekani ilitoa tahadhari za usalama kwa Wamarekani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba kuharibiwa na maandamano ya vurugu.
Makundi ya haki za binadamu, vyama vya upinzani na UN yamesema mamia ya watu huenda waliuawa katika mapigano hayo, ingawa serikali inapinga takwimu hizo kama zilizotiwa chumvi.
ZINAZOFANANA
Wanafunzi 937,581 wachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza, wasichana vinara
Hofu ya D9 yakimbiza watu, bidhaa zakimbiliwa
Ujumbe umefika, watawala wamepotezea