Bunge la EU
HATMA ya Tanzania, kutengwa na ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya (EU), sasa umebaki mikononi mwa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya – chombo cha mwisho – kwa maamuzi hayo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Bunge la Ulaya lilipitisha kwa wingi wa kura, Azimio linaloziagiza nchi wanachama na jumuiya hiyo kwa ujumla, kusitisha misaada yake ya kimaendeleo nchini na mchango wake kwenye Bajeti Kuu ya Serikali.
Mkutano wa Kamisheni ya Ulaya, utakaoamua “kuichinjia baharini Tanzania,” ama kupuuza maamuzi ya bunge lake, utaongozwa na Ursula von der Leyen, rais wa kamisheni hiyo.
EU inaituhumu serikali kwa ukiukaji wa haki za binadamu kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba 2025 na kuwapo mazingira hatarishi ya kisiasa nchini.
Kwa mujibu wa taratibu za EU, pamoja na kwamba Azimio la Bunge la Ulaya ni kali, halikatishi moja kwa moja ufadhili wake kwa taifa husika.
Uamuzi wa mwisho juu ya jambo hilo, upo mikononi mwa Kamisheni ya Ulaya.
Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa kamati za bunge na Bunge lenyewe inapowasilisha hoja inayoungwa mkono kwa ukubwa kama ilivyokuwa kwenye hoja ya Tanzania, Kamisheni nayo huchukua mkondo huo huo.
“Kazi ya Bunge la Ulaya ni kushauri na kutoa maamuzi ambayo hayana nguvu kisheria, ingawa yana mantiki na yanafikisha ujumbe kidiplomasia,” ameeleza mmoja wa wachambuzi wa uchumi na kidiplomasia nchini.
Serikali ya Tanzania ilitarajia kupokea kutoka EU, msaada wa kifedha wa Euro 156 milioni (takribani Sh. 438.7 bilioni), kwa ajili ya miradi ya maendeleo chini ya mpango wa NDICI–Global Europe.
Mabilioni ya shilingi yalipangwa kuingizwa kwenye bajeti ya maendeleo.
Katika mwaka wa fedha wa 2024/25, bajeti ya maendeleo ilikuwa takribani Sh.15 trilioni (takribani dola za Marekani 5.8 bilioni), Sh. 438 bilioni; karibu asilimia 3 ya bajeti nzima ya maendeleo, inaitegemea kutoka kwa washirika wa kimataifa.
Uhusiano wa Tanzania na EU umedumu kwa miongo kadhaa, ukijengwa juu ya misaada, mikopo nafuu, ushirikiano wa kibiashara na miradi ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii.
Kwa miaka mingi, EU imekuwa mmoja wa wadau wa maendeleo na wafadhili wakubwa nchini, ikifadhili sekta za utawala bora, nishati, kilimo, miji, haki za binadamu na mageuzi ya kiuchumi.
Mamilioni ya euro yamekuwa yakiingia kupitia miradi ya moja kwa moja ya serikali na kupitia asasi za kiraia.
Pendekezo la sasa la kusitisha ufadhili linatazamwa kama ishara nzito ya kisiasa, yenye athari za kifedha na kiuhusiano ambazo haziwezi kupuuzwa.
Kupitishwa kwa azimio hili, ambalo limeungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge wa Ulaya, ni hatua inayoashiria msimamo mkali wa Bunge hilo huko Brussels, Ubelgiji kuhusu mwenendo wa kisiasa nchini Tanzania.
Pamoja na kutaka kusitishwa kwa misaada ya kifedha, Bunge hilo limesisitiza wito wake wa kufanyika kwa uchunguzi huru wa madai ya mauaji, kupotea kwa watu na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu uliofuata uchaguzi wa 2025, likisema kwamba hali hiyo “haiendani na misingi ya utawala wa sheria. ”
Aidha, Bunge hilo limetaka kuachiwa huru kwa kiongozi wa upinzani nchini, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini, kuondolewa kwa adhabu ya kifo na kusitishwa kwa misaada ya kifedha ya moja kwa moja kwenda kwenye mamlaka za Tanzania na kuelekezwa zaidi kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs).
Hii si mara ya kwanza kwa Bunge hilo kuchukua msimamo kama huu.
Mei mwaka huu, Bunge hilo, lilipitisha azimio lililoitaka Serikali ya Tanzania kumwachilia huru Lissu bila masharti na kukomesha kile ilichoita, “ukamataji na unyanyasaji dhidi ya wapinzani.”
Katika mantiki ya kidiplomasia, huu ni ujumbe kwa Tanzania kwamba uhusiano wake na EU umejengwa juu ya misingi inayotakiwa kuheshimiwa, sio tu maslahi ya kiuchumi.
Pamoja na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameunda Tume kuchunguza matukio ya 29 Oktoba 2025, Bunge la Ulaya linasema, “Uchunguzi huo, ni sharti ufanywe na taasisi huru kutoka nje na zinazoaminika.”
Uamuzi huu mchungu dhidi ya Tanzania, ulitarajiwa mapema na Serikali.
Akizungumza Dodoma wakati wa kuapisha mawaziri wake, wiki mbili zilizopita, Rais Samia Suluhu Hassan, alikiri kwamba matukio ya yaliyoendana na ghasia za uchaguzi mkuu yanaweza kuathiri uwezo wa Tanzania kupata mikopo na ufadhili wa kimataifa.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, hatua ya Bunge la Ulaya ni ishara ya mabadiliko katika namna jumuiya za kimataifa zinavyoitazama Tanzania baada ya uchaguzi wa 2025.
ZINAZOFANANA
Ulimwengu waisakama Tanzania matukio ya Oktoba 29
Bunge la Ulaya lapitisha maazimio tisa dhidi ya Tanzania
Wanajeshi wa Marekani wapigwa risasi karibu na Ikulu ya White House