Rais Umaro Sissoco Embalo
RAIS Umaro Sissoco Embaló amepinduliwa na maafisa wa kijeshi baada ya milio ya risasi kusikika katika mji mkuu, Bissau kwa siku tatu mfululizo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Shirika la habari la BBC limeripoti kwamba Rais huyo ametiwa mbaroni na maafisa wa kijeshi na kwa sasa yupo chini ya ulinzi.
Brigedia Jenerali Denis N’Canha, mkuu wa Brigedi ya kijeshi mjini Bisau amehutubia kupitia televisheni ya taifa na kutangaza kuwa jeshi limechukua madaraka.
Jenerali N’Canha amesema askari wote wa kikosi cha ulinzi cha Rais wamekamatwa pamoja na mawaziri kadhaa.
Kabla ya Jeshi kutangaza mapinduzi hayo, Rais Sissoco alipiga simu kwenye kituo cha televisheni cha France 24 kilichopo Ufaransa kwa sauti ya kutetemeka na kusema: “Nimewekwa chini ya ulinzi, nimeondolewa madarakani” kabla ya simu hiyo kukatwa ghafla.
Guinea-Bissau ilikuwa ikisubiri matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili, ambapo mgombea mkuu wa upinzani Fernando Dias alienguliwa katika orodha ya wagombea ili kumfanya Rais Umaro ashinde kirahisi.
Jenerali N’Canha ametangaza kufutilia mbali matokeo ya awali ya uchaguzi yaliyoonyesha kumpa ushindi Rais Umaro kwa zaidi ya asilimia 90 na amesema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu mkubwa.
Jenerali N’Canha ametangaza kufunga mipaka ya nchi, huku akiwataka wananchi wabaki watulivu. Pia ameeleza kuwa Jeshi litaongoza nchi hiyo kwa muda mfupi ili kurejesha hali ya utulivu kabla ya kuandaa uchaguzi huru na wa haki.
Rais Umaro alikuwa Rais wa kwanza Afrika kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan baada ya matokeo ya uchaguzi wa Tanzania kutangazwa. Kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter (X) Rais Umaro alipost picha akiwa na Rais Samia na kuandika: “Napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Rais Samia Suluhu kwa kuchaguliwa tena. Ushindi huu ni ushahidi wa imani ambayo wananchi wa Tanzania wamempa na ni kielelezo cha dhamira yake thabiti ya kuendeleza na kustawisha Tanzania.”
ZINAZOFANANA
Maswali tata ya Wahariri kwa Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba
Rais wa zamani wa Brazil, anaanza maisha mapaya gerezani
Vyombo vya habari vimesifiwa au vimedhihakiwa?