Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila
KANISA Katoliki, Jimbo Katoliki la Musoma, limewataka waumini wake na viongozi wa dini nchini, kutojiingiza kwenye mijadala ya matusi, lawama na kejeli. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).
Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila, amesema viongozi wa madhahebu ya kidini nchini hawapaswi “kubeza imani za wengine.”
Ameongeza, “Njia ya Kristo ni ya upole, uvumilivu, huruma na kutanguliza haki.” Ameongeza, “Migogoro na kejeli haviwezi kuizima nguvu ya ukweli.”
Ametoa kauli hiyo, kufuatia matamko yanayoibuka kupitia wanaojiita, “Wahadhili wa Kiislamu nchini,” waliojivika utukufu wa kutetea serikali.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba, kumeibuka matamko kutoka taasisi kadhaa za Kikristo na Kiislamu kuhusu matukio ya wakati na baada ya uchaguzi huo, uliosababisha mamia ya watu kupoteza maisha.
Baadhi ya kauli zimelishambulia Kanisa Katoliki kwa kile kilichoelezwa kuwa ni uchochezi dhidi ya amani ya nchi na kuzuia maendeleo ya Waislamu.
Kauli ya Askofu Msonganzila imejiri huku baadhi ya viongozi wa madhehebu ya Kiislamu, waking’ang’aniza hoja ya udini kutetea mauaji ya raia ya 29 Oktoba mwaka huu.
Askofu Msonganzila amesema: “Hamna sababu ya kuijibu, ni kuinyamazia tu wakati mwingine watu wakisema sisi tumeenda shule sio zamani, kwani kwenda shule ni shida?
Shida ni kusoma, shida ni kuelimika, sasa kuzozanazozana katika misingi hiyo haina haja- ni kunyamaza kama Kristo aliyedhihakiwa: Wewe si ni mwana wa Mungu Jiokoe basi nafsi yako, Nyamaza kimya endelea kusali,” amefafanua.
Askofu huyo amesema, nguvu ya maneno ya kupotosha haiwezi kuzidi uzito wa maadili, utu, na dhamira njema ya Kanisa.
Ameonya kuwa matusi na vitisho ambavyo vimekuwa vikitolewa haviwezi kubadilisha msingi wa imani wala wajibu wa viongozi wa dini kusimama katika kweli.
Amesema, mahangaiko yakitokea wasiogope kwa sababu ndio Kristo amepitia njia hiyo,
Amesema, “Kanisa Katoliki linaweza likateseka kwa njia za namna hiyo hiyo na matishio mbalimbali: Umemwaga ugali tutamwaga mchuzi, tutawakatakata- tusiogope Mungu yupo.”
Baadhi ya taasisi za Kiislamu nchini, zikiongozwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), zimekuwa ziituhumu Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), kuisakama Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Wanasema, Kanisa Katoliki linampinga Rais Samia kwa kuwa ni Muislamu na kwamba wanalituhumu Kanisa kupinga Mahakama ya Kadhi; jambo wanalodai linakwamisha maendeleo ya waislamu.
ZINAZOFANANA
Washtakiwa 57 wa uhaini waanza kuachiliwa
Thabo Mbeki: Tanzania inahitaji mwanzo mpya haraka
Ripoti yetu kuhusu Tanzania imezingatia weledi – CCN