November 25, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Heri ya siku ya kuzaliwa kwa Polepole, ni siku 51 tangu ametekwa

Humphrey Polepole

 

IKIWA ni siku 51 sawa na saa 1,224, dakika 73,440 tangu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, kuripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana, leo ni kumbukizi ya siku yake ya kuwzaliwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Leo tarehe 25 Novemba ndiyo siku ya kuzaliwa kwa mwanadiplomasia huyo ambaye mpaka leo kitandawili cha wapi alipo hakijateguliwa mpaka leo Mama yake mzazi Anna Mery hajaacha kumlilia mwanawe.

Hadi sasa, taarifa hizo zimeendelea kutawala mijadala mitandaoni bila kuwepo uthibitisho rasmi kutoka kwa vyombo vya dola au familia yake, wapi alipo Polepole.

Kila siku imekuwa ikizua maswali mapya, mijadala mipya na hisia tofauti na wengine wakionesha wasiwasi juu ya usalama wake, huku wengine wakisisitiza umuhimu wa kupata taarifa sahihi badala ya kutegemea tetesi.

Ukimya wa mamlaka umeongeza sintofahamu na kuifanya sakala hilo kuendelea kuchukua kasi kama moja ya matukio yaliyozua gumzo kubwa zaidi nchini katika wiki za karibuni.

Siku 51 baada ya kutekwa nyumbani hali ya Polepole hakuna anayejua. Tangu tarehe 6 Oktoba 2025, stori isiyothibitishwa imeanza kusambaa mtandaoni ikidai kuwa aliyekuwa balozi huyo, ametekwa nyumbani kwake Ununio wilaya ya kinondoni jijini Dar es Salaam, na watu wasiojulikana.

Hali hiyo imechochea hofu, sintofahamu, na mijadala mkali mitandaoni huku wananchi wakitaka uthibitisho rasmi kutoka kwa vyombo vya dola.

Kwa zaidi ya wiki saba sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu hali yake, hatua za polisi, au hatua za serikali kushughulikia tukio hili. Kila taarifa mpya inayotokea kwenye mitandao huongeza zaidi gumzo la umma na kuibua maswali kuhusu usalama wa watu wenye hadhi ya kisiasa au kiutawala nchini.

Humphrey Polepole alizaliwa tarehe 25 Novemba 1981, huko mjini Tabora, akiwa mtoto wa nne kati ya sita wa Anna Mery na Hezron Polepole, aliyekuwa fundi wa magari.

Polepole amepata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Mbuyuni na akapata masomo yake ya sekondari katika shule za Azania na Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Polepole ni Mwanasiasa aliyeshika nafasi mbalimbali za uongozi, katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali hadi pale alipochaguliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, eneo la Karibe, Amerika ya Kati.

About The Author

error: Content is protected !!