KITUO cha habari cha kimataifa cha CNN kimesisitiza kuwa ripoti yake juu ya matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025 nchini Tanzania, imejengwa kikamilifu juu ya ushahidi; hakikuchapisha taarifa yoyote ambayo haikuweza kuthibitishwa. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na SABC News, mwandishi wa habari wa CNN, Larry Madowo alisema, uchunguzi wao ulifanywa kwa kutumia mahojiano na zaidi ya Watanzania 100, uchambuzi wa kitaalamu wa sauti, ulinganifu wa video, na picha za satelaiti ili kufuatilia matukio ya vurugu, vifo na madai ya makaburi ya pamoja.
Alisema, “Tulifanya kazi kwa umakini mkubwa. Tulihakiki kila ushahidi tuliyoupata na hatukutohoa taarifa yoyote bila kuwa na uthibitisho wake.”
Aliongeza, “Tuliikagua kila video na kila sauti, na ushahidi unaonesha wazi kuwa raia wasiokuwa na silaha walipigwa risasi na polisi au watu waliokuwa na bunduki.”
Madowo alisema hakuna mtu wala mamlaka yoyote iliyokanusha ukweli wa taarifa zao tangu ziwekwe hadharani.
“Tangu tulipotangaza ripoti hii, hakuna yeyote aliyesema kuwa tulidanganya au tuliandika taarifa za uongo,” ameeleza Madowo.
Kauli ya mwandishi huyo mahiri wa habari za uchunguzi imekuja siku moja, baada ya Serikali ya Tanzania, kudai kuwa ripoti hiyo, imeegemea upande mmoja.
Gerson Msigwa, Msemaji wa Mkuu wa Serikali, amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kwamba “ripoti hiyo, imekosa weledi, haina minzania na imeegemea upande mmoja.”
Alisema, uhakiki wa maudhui ya CNN unaendelea lakini akasisitiza kuwa shirika hilo “halikutoa nafasi sawa kwa upande wa serikali.”
Amemtuhumu mwandishi wa CNN kuwa hakuwasiliana na mamlaka za Tanzania na alitumia picha za simu bila kuzingatia taratibu za kiweledi.
“Hawakufuata maadili. Uandishi wa habari unatakiwa kuwa wa pande zote. Hatusemei vifo vilivyotokea; sote tumesikitishwa. Lakini kwa nini kutengeneza maudhui yanayoongeza maumivu na hasira kwa wananchi?” alihoji Msigwa.
Akaongeza, “Ni kinyume cha maadili kuchapisha picha mbaya ambazo hazijathibitishwa ipasavyo. Tume imeundwa kuchunguza na itatoa ripoti. Tunatoa wito CNN waje upande wa serikali wasikilize, na wachapishe taarifa zenye uwiano na ukweli.”
Mbali na CNN, Msingwa amevitaja vyombo vya habari vya CNN, Aljazeera, BBC na DW, kwamba vimekuwa vikichapisha habari za upande mmoja na zenye nia ovu kwa Tanzania.
Kauli ya Msigwa inajiri kufuatia ripoti za mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania; pamoja na kubinywa kwa mtandao uliovizuia vyombo vya habari vya ndani kuripoti kilichotokea, vyombo vya kimataifa vilifanikiwa kuandaa taarifa za ghasia hizo za uchaguzi hatua ambayo imezua shutuma kutoka kwa serikali.
Maandamano hayo ya kutaka mabadiliko mbalimbali ikiwemo mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki, yameelezwa kuwa miongoni mwa machafuko makubwa zaidi nchini Tanzania tangu taifa hilo lipate uhuru wake, tarehe 9 Desemba 1961.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, mamia ya watu wanaripotiwa kufariki dunia.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, alinukuliwa akisema, serikali haina idadi kamili ya watu waliofariki na uhalibifu ulioyotokea.
ZINAZOFANANA
Mzimu wa Oktoba 29 unavyoitesa Serikali
Serikali yavikosoa vyombo vya habari vya kimataifa
Rais Mwinyi azindua miradi ya nyumba