RAIS Samia Suluhu Hassan, ametetea Tume Huru ya Uchunguzi aliyounda kuchunguza anachoita, “matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi wa 29 Oktoba 2025.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tume yake mjini Dodoma, leo tarehe 20 Novemba, Rais Samia alisema, ana matumaini makubwa na tume aliyoiunda. Amesema, ni muhimu uchunguzi wa awali kufanywa na tume ya ndani kabla ya kuhusisha timu kutoka nje.”
Ametoa kauli hiyo, siku moja baada ya baadhi ya vyama vya upinzani Tanzania, vikiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF), kupinga uteuzi wa tume hiyo.
Vimesema, tume iliyoundwa siyo huru, na kwamba baadhi ya wajumbe wanahusishwa na matukio ya vurugu yaliyotokea.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, alifika mbali zaidi na kusema haiwezekani mtuhumiwa akajichunguza mwenyewe na kutarajia haki.
Alisisitiza umuhimu wa kuundwa kwa tume ya kimataifa yenye uwezo na weledi wa kuchunguza kwa haki, msimamo ambao pia umetolewa na ACT-Wazalendo na CUF.
Wengine wanaopinga kuundwa kwa tume hiyo, ni Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wakieleza kuwa kilichofanyika ni ghiliba dhidi ya wananchi.
Akijibu hoja za wapinzani wa tume yake, Rais Samia amesema ana imani kubwa na uwezo wa tume; anatarajia itautoa majibu sahihi yatakayosaidia taifa kusonga mbele.

Alisema, “…nimewasikia wenzetu wa upinzani wanasema hawana imani na tume yoyote ya ndani, wanataka tume itoke UN (Umoja wa Mataifa), AU (Umoja wa Afrika au Umoja wa Ulaya (EU). Lakini mimi nina imani sana na tume hii, kwa ubobezi na uzoefu wenu. Natumaini mapendekezo yenu yatatutoa hapa tulipo na kutupeleka mbele.”
Katika maelezo yake, Rais Samia hakukubali wala kupinga hoja ya kuundwa kwa tume ya kimataifa, badala yake alisisitiza kuwa tume ya ndani iwe ya kwanza kufanya kazi ili timu zitakazokuja kutoka nje zishirikiane na watoa taarifa waliokwishaanza uchunguzi.
“Kwenye hili lililotokea nikaona kwamba kabla ya kuletewa tume kutoka nje tuwe na tume yetu wenyewe ya ndani, ifanye kazi na za nje zikija zitakuja kuzungumza na tume mwenzao ambao walishaanza hiyo kazi,” ameeleza.
Kwa mujibu wa Samia, tume hiyo utafanya kazi kwa muda wa miezi mitatu, ambapo pamoja na mengine, itachunguza chanzo cha kadhia na sababu halisi zilizoibua vurugu, kutathimini madai ya vijana walioingia barabarani.
Kazi nyingine ya tume hiyo, ni kubaini walikuwa wanadai haki gani, kuchambua matamshi ya vyama vya upinzani, ikiwemo kauli za uchochezi zinazodaiwa kutolewa kabla ya uchaguzi.
Mengine, ni kuangalia uhusiano kati ya vyama vya siasa na Tume ya Uchaguzi, kuchunguza mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ya ndani na nje katika matukio ya 29 Oktoba 2025, kutathmini kama kulikuwa na njia mbadala zaidi ya maandamano, uvunjifu wa amani, na vitendo vya uchomaji, ili kushughulikia changamoto kati ya tume, vyama vya siasa na serikali.

Rais Samia alitangaza kuundwa kwa Tume ya Rais, wiki tatu baada ya maandamano ya siku tatu ya kuanzia siku ya uchaguzi wa 29 Oktoba, yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa na uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Uchaguzi mkuu wa Tanzania, uliogubikwa na ghasia na mauaji, unatajwa na wangalizi wa kimataifa, wakiwamo Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika, kuwa uligubikwa na udanganyifu.
Maandamano hayo yaliyolenga kushikiniza kuwapo mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki, yamepoteza uhai wa watu ambao idadi yao haijatajwa, huku zaidi ya vijana 500 wakifunguliwa kesi ya uhaini.
Waandamanaji waliharibifu mali za umma na binafsi, ikiwemo ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilizokuwa zimechomwa moto.
Kwa takribani miaka 30 sasa, wananchi wamekuwa wakitaka kuwapo mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi na ujio wa Katiba Mpya.
Wamekuwa wakitaka viongozi wapatikane kwa njia ya haki, kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi; mgombea binafsi, misingi na miiko ya uongozi, Tume ya Haki za Binadamu na maadili ya viongozi wa umma.
Lakini serikali tokea utawala wa Alli Hassan Mwinyi hadi Samia, wamepuuza madai hayo na kuamua kubaka kila uchaguzi unaofanyika nchini.
Madai ya kubakwa uchaguzi yalianza kushika kasi baada ya uchaguzi mkuu 2015, ambapo mamia ya wagombea upinzani walioshiriki chaguzi za marudio, baada ya kujiuzulu waliokuwa wanashikilia nafasi hizo, kupitia mradi mahususi wa “kuunga mkono juhudi,” walienguliwa.
ZINAZOFANANA
Serikali yaanza kuonja kibano cha kimataifa
Tukiacha kubaka uchaguzi, tutakuwa salama
Zitto Kabwe azinduka usingizini