November 17, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mwanajeshi wa Marekani akamatwa na mabomu Tanzania

Msemaji wa Polisi, DCP David Misime

 

JESHI la Polisi Mkoa wa Polisi Tarime- Rorya, limesema limemkamata Charles Onkuri Ongeta, mwenye uraia pacha wa Kenya na Marekani, katika eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya, Sirari. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tarime …(endelea).

Charles Onkuri Ongeta (30), mwanajeshi wa Jeshi la Marekani, mwenye cheo cha Sajenti, amekamatwa akiwa na mabomu manne ya kurushwa kwa mkono, aina ya CS M68, akitokea Kenya kuingia Tanzania.

Anatuhumiwa kuingia nchini na mabomu hayo ya mkononi kinyume cha sheria.

Taarifa ya jeshi hilo imesema, tukio hilo limetokea Jumapili, tarehe 16 Novemba 2025, majira ya saa 6:00 mchana katika eneo la mpakani Sirari.

“Kwa mujibu wa sheria Tanzania za umiliki wa silaha, mabomu hayo, hata kama angeomba kibali cha kuingia nayo nchini, asingeruhusiwa kuyaingiza,” imeeleza taarifa hiyo.

Polisi wamesema, uchunguzi wa suala hilo unaendelea, ikiwemo kukusanya ushahidi na kumhoji mtuhumiwa, kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.

Mtuhumiwa aliingia nchini Tanzania, kutokea Kenya kwa gari aina ya Toyota Landcruiser lenye namba za usajili KDP 502.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakati askari wanafanya ukaguzi wa mpakani, walikuta mabomu hayo manne ya mkononi aina ya CS M68, ambayo ni silaha zinazodhibitiwa kisheria na ambazo hata kwa kibali maalum haziruhusiwi kuingizwa nchini.

About The Author

error: Content is protected !!