RAIS wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amemfuta kazi Makamu wa Rais na Naibu Kiongozi wa chama tawala, Benjamin Bol Mel.
Hatua hiyo imeashiria kuvunjika kwa uhusiano wa karibu uliokuwepo kati ya viongozi hao wawili, huku Bol Mel akitajwa kwa muda mrefu kuwa mrithi anayempenda Kiir mwenyewe. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Kiir pia amemfuta kazi Gavana wa Benki Kuu na Mkurugenzi wa mamlaka ya mapato, ambao wote wanatajwa kuwa washirika wa karibu wa Bol Mel. Mabadiliko haya yamekuja wakati taifa hilo linaendelea kukumbwa na sintofahamu kuhusu urithi wa madaraka na hofu ya kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, hatua ya Kiir ilitanguliwa na hali ya taharuki mjini Juba baada ya kikosi cha ulinzi katika makazi ya Bol Mel kupunguzwa ghafla kabla ya tangazo hilo kutolewa.

Bol Mel, ambaye alipandishwa cheo cha Jenerali, Septemba mwaka huu, ameondolewa pia katika cheo hicho.
Amekuwa akituhumiwa kwa vitendo vya ufisadi mkubwa, ambapo ripoti ya Umoja wa Mataifa mwaka huu ilidai kampuni zinazohusishwa naye zililipwa zaidi ya dola
1.7 bilioni, kwenye miradi ya ujenzi wa barabara ambayo haikukamilika.
Marekani imekuwa ikimuweka Bol Mel chini ya vikwazo tangu mwaka 2017 kwa madai ya kutumia vibaya madaraka na kuwa mshauri wa kifedha wa karibu wa Rais Kiir, madai ambayo Ikulu ya Juba imeyakanusha.
ZINAZOFANANA
Umoja wa Afrika: Uchaguzi wa Tanzania ulivurugwa
Mambo matano makubwa kuhusu Raila
Raila Odinga alikuwa mwanaharakati wa demokrasia – Barack Obama