ALIYEKUWA mgombea urais Visiwani Zanzibar, Othman Masoud Othman (OMO), amewataka wafuasi wake, kupigania alichoita, “Zanzibar yenye heshima.” Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Pemba…(endelea).
Amesema, “…sisi siyo watu wa kubezwa na hatutakubali kuburuzwa na kudharauliwa tena.” Akaongeza, “huu ni wakati wa kila Mzanzibari kutambua wajibu wake katika kutetea haki.”
Mwenyekiti huyo wa chama cha ACT-Wazalendo, ametoa kauli hiyo, leo kisiwani Pemba, wakati akizunguma na wananchi, katika ziara yake maalum ya siku nne kisiwani humo, inayolenga kuimarisha mshikamano wa wanachama na kufufua ari ya kisiasa ndani ya chama chake.
Amesema, ACT- Wazalendo, kitaendelea kusimama kidete katika kudai uchaguzi huru, haki na shirikishi, ili wananchi wafanye maamuzi yao wenyewe kuhusu mustakabali wa taifa lao.

Makamo huyo wa rais katika serikali iliyopita, ameonya kuwa nchi inaweza kuingia katika machafuko, ikiwa haki na misingi ya demokrasia itaendelea kupuuzwa, kauli iliyopokelewa kwa shangwe na wafuasi wake.
Ziara hiyo ni ya kwanza kwa kiongozi huyo, tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba, imekuwa na hamasa kubwa, huku maelfu ya wafuasi na wanachama wa ACT Wazalendo wakijitokeza kwa wingi kumpokea kiongozi wao, katika ofisi za mratibu wa chama eneo la Gombani, wilaya ya Chake Chake.
Akiongea kwa hisia kali, Othman alisema, “Tunataka Zanzibar yenye uwazi, usawa na uadilifu. Tunataka demokrasia inayojengwa juu ya misingi ya heshima na haki kwa wote. Huu ndio urithi tunaoutaka kwa vizazi vijavyo.”

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wanachama wa ACT- Wazalendo kwa kuendelea kuwa na imani na chama hicho na kuwataka kuendeleza juhudi za kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa umoja, maendeleo na uadilifu wa kisiasa.
Othman anatarajiwa kutumia ziara hiyo, kukutana na viongozi, wanachama na wananchi, ili usikiliza changamoto zinazowakabili.
Mbali na kukutana na wananchi, Othman anatarajia kuitumia ziara hiyo, kufanya tathimini ya kilichotokea katika uchaguzi huo.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imemtangaza Dk. Hussein Ali Mwinyi (CCM), kuwa mshindi wa uchaguzi huo. Alipata wa urais katika visiwa hivyo.
ZINAZOFANANA
Watu 300 waliokamatwa kwenye maandamano Kilimanjaro waachiwa
ACT yatia shaka kifo cha diwani wao aliyekuwa mahabusu
Mawakili wa Heche walishtaki Jeshi la Polisi