November 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

ACT yatia shaka kifo cha diwani wao aliyekuwa mahabusu

Marehmu Dafroza Jacob

 

MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, mkoa wa Mara, Charles Mwera, ametia shaka juu ya kifo cha ghafla cha aliyekuwa mgombea udiwani wa Kata ya Sirari, wilaya ya Tarime, mkoani Mara Dafroza Jacob (46) akiwa chini ya jeshi la polisi kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano na vurugu. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).

Mwera amenukuliwa alipokuwa akiongea na waandishi wa habari na kusema walipofanya jitihada za kumuombea dhamana walielezwa kuwa haiwezi kutolewa kwa siku hiyo kwakuwa bado kuna maafisa kutoka Rorya wanaosubiriwa kuja kufanya mahojiano na mtuhumiwa, anasema siku ya pili (tarehe 5 Novemba 2025) jioni ndipo alipopata taarifa kutoka kwa OCD kuwa kada wao aliugua ghafla, akakimbizwa Hospitali na ndipo umauti ulipomfika

“Nilipoongea na OCD ndipo akanieleza kwamba Dafroza aliugua ghafla, akakimbizwa Hospitalini,ndipo alipokuwa ameshikwa, sasa nilipotaka kumjulia hali na kumuomba OCD anipe niongeenae ndipo akaniambia kuwa mtuhumiwa aligua ghafla na kukimbizwa Hospitalini, na OCD akaniambia kuwa kwa wakati huo hayuko tena Sirari yupo Tarime, muda mfupi baadaye ndipo nikapata taarifa kuwa amefariki,” amesema Mwera.

Amesema Dafroza alikamatwa na Jeshi la Polisi tarehe 4 Novemba 2025 na taarifa za kifo alipokea tarehe 5 Novemba 2025 akiwa hospitalini akipatiwa matibabu baada ya kuumwa ghafla.

Mwera amendelea kueleza kuwa, awali baada ya kupatiwa taarifa kuwa Dafroza anaumwa na amekimbizwa Hospitali kwa matibabu waliendelea kusisitiza kuwa ni busara angepatiwa dhamana ili wakamuuguze kwanza lakini bado wakajibiwa kuwa kwa sasa kuna uchunguzi unafanyika dhidi ya tuhuma zinazowakabili

“Sisi kama chama kwakweli tunalaumu hiki kilichotokea, tutakaa, tutaangalia modarity ya kifo hicho kimetokeaje ili niweze kusema kitu, maana muda huu (wakati anaongea na waandishi ) sijafika hapo, sijafika Sirari niweze kujuwa kwamba kimetokeaje hicho kifo, nini kimesababisha kifo chake, lakini yale madai ya kwamba yule dada ndio alikuwa anadhamini maandamano hiyo ndio kitu cha kusikitisha kwakweli,” amesema Mwera.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya kupitia kwa Kamanda wake, SACP Mark Njera, limethibitisha kutokea kwa kifo hicho ambapo kupitia taarifa yake ya Novemba 05.2015 imeeleza kuwa marehemu Dafroza Kokwangua Jacob (Mama Frank) amefariki majira ya saa 07 mchana alipokuwa akiandikwa maelezo yake kutokana na tuhuma zilizokuwa zinamkabili, ambapo aliugua ghafla na kulazimika kukimbizwa Hospitali kwa matibabu.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, wakati akiwa anapatiwa matibabu ndipo alipofariki Dunia, Jeshi hilo limesema uchunguzi utafanyika kwa kushirikisha wataalamu wa uchunguzi wa vifo ili kubaini chanzo cha kifo chake.

About The Author

error: Content is protected !!