October 22, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Lissu aibwaga tena serikali, Heche akamatwa

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameipigwa mweleka serikali, baada ya Mahakama Kuu, jijini Dar es Salaam, kuridhia pingamizi aliloweka dhidi ya shahidi wa Jamhuri. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akisoma uamuzi wa shauri hilo, leo Jumatano, tarehe 22 Oktoba, Jaji Dunstan Ndunguru, ameeleza kuwa hoja ya mshitakiwa (Lissu), kwamba shahidi huyo, hakuorodheshwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kama mmoja wa wataalamu wa video.

Majaji wengine kwenye kkesi hiyo, Na. 19605 ya mwaka 2025, James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Katika kesi hiyo, Jamhuri ilitaka kumtumia shahidi namba tatu, Samwel Kaaya, aliyekuwa ametambulishwa kama mtaalamu wa picha, kuwasilisha video yake mahakamani na kupokelewa kama sehemu ya kielelezo.

Kwa uamuzi huo, kielelezo hicho muhimu kwenye shauri hilo, sasa hakitaweza kuingizwa mahakamani.

Tayari mashahidi wawili wa Jamhuri wameshakamalisha kutoa ushahidi wao – Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, George Wilbard Bagyemu na John Kaaya, ofisa wa polisi anayefanya doria mitandaoni ili kubaini uhalifu wa kimtandao.

Katika hatua nhyingine, Makamu mwenyekiti wa chama hicho (Bara), John Heche, amekamatwa maeneo ya mahakamani, wakati alipofika maeneo hayo, kufuatilia kesi dhidi ya mwenyekiti wake.

Hadi anakamatwa polisi walikuwa hawajaeleza sababu za kumshikilia mwanasiasa huyo machachari anayeongoza Chadema kwa ufanisi katika kipindi kigumu.

Hata hivyo, mwishoni wa wiki, Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania, ilimtuhumu Heche kuvuka mpaka na kuingia nchini Kenya kinyume cha taratibu, madai ambayo mbunge huyo wa zamani wa Tarime Vijijini, aliyekanusha vikali.

Heche alifika mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwa lengo la kutaka kusafiri kuelekea nchini Jirani, kuhudhuria msiba wa Raila Odinga, Waziri mkuu wa zamani wa taifa hilo, aliyezikwa Jumapili iliyopita, kijijini kwake, Bondo.

Katika barua yake iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Orange Democratic Movement (ODM), Heche alisema, ameshindwa kuhudhuria mazishi ya kiongozi mkuu wa chama hicho, kutokana na kuzuiwa kwenye mpaka wa Isibania One Stop, wilayani Tarime, mkoani Mara na maofisa wa Uhamiaji.

Amesema, viongozi wa chama chake, waliandaa msafara wa viongozi wake wakuu, kuhudhuria “mazishi muhimu ya mwanasiasa mkongwe nchini Kenya,” lakini kwa masikitiko makubwa hawataweza kufanya hivyo.

About The Author

error: Content is protected !!