
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira amesema kazi kubwa aliyoifanya mgombea urais wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka minne na nusu aliyoiongoza nchi, ndiyo inayowafanya Watanzania wampe miaka mitano mingine ya kuongoza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kishapu … (endelea).
Amesema kukamilisha miradi mikubwa ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere na Daraja John Pombe Magufuli (Kigongo-Busisi) ni ushahidi wa uimara na uwezo wake katika kusimamia maendeleo ya nchi.
Wassira alitoa kauli hiyo leo tarehe 19 Oktoba, 2025 alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga, akiwa katika ziara za kusaka ushindi kwa mgombea urais wa CCM na wagombea waliosimamishwa na chama hicho kuwania ubunge na udiwani.
“Rais Samia alipokea kijiti (ungozi) nchi ikiwa inakabiliwa na miradi mikubwa ambayo ni kujenga reli, reli ya kati na haikusimamiwa na wazungu walioajiriwa, mtu aliyekuwa anasimamia kwa niaba ya rais kujenga reli ya kati yupo hapa, ndugu Kadogosa (Masanja Kadogosa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli ‘TRC’).
“Ilikuwa haijafika Morogoro, lakini Kadogosa ametoka ameiacha Makutupora, kilometa 722 kutoka Dar es Salaam lakini Kadogosa ameondoka ameacha na wakandarasi wanaendelea wengine kutoka Mwanza kwenda Isaka na inaendelea, hata nyie mkienda Mwanza mnaiona na ipo inayotoka Isaka kwenda Tabora na kutoka Makutupora kwenda Tabora na inatoka Tabora kwenda Kigoma reli pia inatoka Kigoma kwenda Burundi ili watu wa DRC walete madini Dar es Salaam kupitia reli.
Aidha, amesema Rais Samia amefanya kazi kubwa yenye kutukuka kusimamia ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere hadi kukamilika kwake na kuiwezesha nchi kuwa na umeme wa kutosha.
“Sasa nchi ina umeme zaidi ya mahitaji kwa sababu Rais Magufuli (Rais wa Awamu ya Tano hayati Dk. John Magufuli), aliacha mradi wa bwawa akalipa jina la Mwalimu Julius Nyerere kule Rufiji, limesimamiwa, lilikuwa asilimia 30 wakati Magufuli anatutoka, asilimia 70 zimejengwa kwa miaka minne na limekamilika, leo hii nchi ina umeme mwingi.
“Mama Samia alitwambia Kazi Iendelee na mimi nawauliza je kazi imeendelea au haikuendelea bila shaka jibu la kila mmoja kazi imeendelea,” alieleza.
Mbali na miradi hiyo, Wassira amesema kuwa Dk. Samia aliachiwa ujenzi wa daraja la John Pombe Magufuli, ujenzi wake sasa umekamilika na linatoa huduma.
Amesema awali ilikuwa inamchukua mtu saa moja kusubiri kuvuka katika eneo hilo, lakini sasa kwa dakika tatu mtu anakuwa ameshavuka “limejengwa, limesimamiwa na Rais Samia.”
Wassira ameeleza kuwa, Rais Dk. Samia ana kipawa cha uongozi ndiyo maana amefanikiwa kuiongoza vema Tanzania licha ya kuchukua uongozi katika mazingira magumu.
“Mungu amegawa vipaji, urais ni Katiba, urais ni sheria, urais ni kanuni na urais ni busara, hakuna mtu anaweza kusimama akatoa ushahidi wa kisayansi kwamba wanamume wana busara zaidi kuliko wanawake, hakuna ushahidi huo. Rais Samia amebarikiwa kipawa cha uongozi.
“Kila mmoja sasa anakubali kwamba Samia amefanya kazi yake vizuri,” amesema.
ZINAZOFANANA
Heche hajaenda Kenya – Chadema
Mpina ndiyo bhasi tena, kesi yake yatupwa
Lissu hajamalizana na shaihidi wa serikali, msiba waahilisha kesi yake