October 2, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

OMO: Nitairejeshea Zanzibar rasilimali zake, Wananchi wafaidike

 

MGOMBEA urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kuwa mara tu baada ya kuingia Ikulu ya Zanzibar, Serikali yake itahakikisha Katiba inarekebishwa ili rasilimali za mafuta na gesi ziwe mali ya Wazanzibari pekee na kuondolewa kabisa kwenye mambo ya Muungano. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema hayo mbele ya maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Shehia ya Pujini, Wilaya ya Chake Chake, ambapo alieleza wazi kuwa Zanzibar haiwezi kubaki maskini ilhali imejaaliwa utajiri mkubwa wa rasilimali za asili.

Alisema haiwezekani Wazanzibari wakaendelea kuwa maskini katika ardhi yao wenyewe wakati tunazo rasilimali ambazo zingeweza kuingiza mabilioni ya fedha.

Alisema Serikali yake itahakikisha mali hizi zinawanufaisha wananchi moja kwa moja.

Othman alisema kisiwa cha Pemba kimebarikiwa kwa bahari yenye mazao mengi lakini wananchi bado wanatumia zana duni kama videu. Aliongeza kuwa bidhaa za baharini kutoka Pemba zinaliwa duniani kote, lakini wananchi wa kisiwa hicho wanaendelea kuishi kwa njaa na umaskini.

Vilevile, alisisitiza kuwa ardhi ya Pemba ni yenye rutuba kila mahali, lakini wananchi wake wametengwa na kukosa uwekezaji wa Serikali.

Akirejea historia, Othman alikumbusha msimamo wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume, aliyekataa mikopo kwa sababu Zanzibar ilikuwa ikijitosheleza.

Aidha, alifichua kuwa hivi karibuni madini mapya yamegunduliwa kisiwani Pemba ambayo yana uwezo wa kutengeneza simu, na pia eneo la Tungamaa – Wete limegundulika kuwa na madini ya dhahabu.

Alisema umasikini wa Pemba si kwa sababu ya kukosa rasilimali, bali ni kwa sababu ya uongozi usiochaguliwa na wananchi, viongozi waliopanda madarakani kwa njia zisizo sahihi na kukosa maono ya kitaifa.

Mgombea huyo alisema kuwa Zanzibar itaendelea kudhulumiwa endapo wananchi hawatafanya uamuzi sahihi. Akahimiza kuwa njia pekee ya kuondoa madhila haya ni kumpa ridhaa ya urais kupitia kura za 29 Oktoba.

Meneja wa kampeni wa ACT-Wazalendo, Ismail Jussa, naye alizungumza katika mkutano huo akisema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM), hakijawahi kushinda kihalali Zanzibar, bali kimekuwa kikitumia dola kupora ushindi wa wananchi.

Alisema wananchi wa Zanzibar wameshachoshwa na dhulma na ufisadi. Ni jukumu la Tume ya Uchaguzi kuhakikisha haki inatendeka.

Aidha alisema safari hii Wazanzibari wako tayari kwa namna yoyote ile kulinda maamuzi yao.

Baada ya mkutano huo, wazee na wananchi wa Pujini walionesha imani kubwa kwa mgombea huyo wa ACT Wazalendo.

Mzee Salim Ali, mmoja wa wazee maarufu wa Pujini, alisema hotuba ya Othman imeonyesha dira ya kweli ya kuwakomboa Wazanzibari.

“Tumemsikiliza kwa makini, huyu ndiye kiongozi tuliyekuwa tukimsubiri. Amezungumza kwa uchungu wa wananchi na ana maono ya kweli ya Zanzibar huru na yenye neema,” alisema.

Mwanamkuu Khamis, mkazi wa Pujini, alisema wanawake na vijana wa Zanzibar wana kiu ya mabadiliko.

“Tunataka rais atakayehakikisha rasilimali zinawanufaisha wananchi wote. Othman ndiye kiongozi sahihi wa zama hizi,” alisema huku akishangiliwa na wenzake.

Wengine walieleza kuwa hotuba ya mgombea huyo imeamsha ari ya kushiriki uchaguzi kwa wingi na kuhakikisha kura zao zinalindwa hadi mwisho.

About The Author

error: Content is protected !!