September 23, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Netanyahu acharuka Pelestina kutambuliwa

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

 

WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa kuanzishwa kwa taifa la Palestina ‘hakutatokea’, akijibu hatua ya mataifa matatu ya Jumuiya ya Madola—Uingereza, Canada na Australia—kuitambua rasmi Palestina kama taifa huru. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa hatua hiyo siku ya Jumapili, Netanyahu alieleza kuwa uamuzi huo unatoa ‘zawadi kubwa kwa ugaidi’ na unahatarisha usalama wa taifa la Israel.

Netanyahu alisisitiza kuwa kwa kipindi chote cha uongozi wake, amepinga vikali kuanzishwa kwa taifa la Palestina, licha ya mashinikizo kutoka kwa jamii ya kimataifa na baadhi ya mataifa washirika wa Israel.

Alibainisha kuwa eneo la magharibi mwa Mto Jordani, ambalo linajumuisha Ukingo wa Magharibi, halitakubaliwa kuwa sehemu ya taifa huru la Palestina kwa vyovyote vile.

Kauli ya Netanyahu imeibua mjadala mkubwa wa kimataifa, hasa ikizingatiwa kuwa nchi zilizotangaza kutambua Palestina zimesema hatua hiyo inalenga kuhimiza suluhisho la amani la mataifa mawili na kusaidia Wapalestina kupata haki yao ya kujitawala.

Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, amepongeza hatua hiyo, akiita ni hatua muhimu kuelekea haki, uhuru na amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati.

About The Author

error: Content is protected !!