
Humphrey Polepole
ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, amekana madai ya Jeshi la Polisi nchini Tanzania, kwamba limemtafuta bila mafanikio. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
“Siyo kweli kwamba jeshi la polisi, limenitafuta sana. Hili siyo kweli. Ningekuwa bado mwanadiplomasia, ningesema hamjasema ukweli. Lakini kwa kuwa mimi siyo mwanadiplomasia, nawaambia mmesema uwongo,” ameeleza balozi huyo wa zamani.
Ameongeza, “Nimekuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na baadhi ya maofisa wa polisi, tena maofisa waandamizi kabisa. Kwa hiyo, kama mngekuwa mnanitafuta na hamjanipata, basi hao maofisa wangewapa mawasiliano yangu na mimi napatikana kwa njia ya simu.”
Polepole ametoa kauli hiyo, leo Alhamisi, tarehe 18 Septemba 2025, katika mazungumzo yake na umma na kuongeza, “…ni kweli mmekuwa mkinitafuta, lakini siyo kwa nia njema.”
Amesema, mara ya kwanza, jeshi hilo lilianza kumtafuta tarehe 13 Julai mwaka huu, ambapo maofisa wa polisi waliobeba silaha za moto, walivamia nyumbani kwake, Masaki jijini Dar es Salaam, kutaka kumkata.
Aliyekuwa katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesisitiza kuwa tarehe Julai 2025, maofisa hao wa polisi walifika nyumbani kwa dada yake, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam na baadaye kuondoka naye.
“Nilifuatilia suala hili kwa kutwa mzima. Nilianza kuriripoti baada ya kuondoka na dada yangu,” amesisitiza Polepole.
Balozi aliyejizulu alisema, anapinga masuala ya utekeaji na kuwa dada yake alitekwa na kuumizwa.
Katika hotuba yake ya leo kupitia mtandao wake wa Facebook na Instagram, Polepole ametaja mambo yote ambayo ameyazungumzia na ambayo polisi wamesema, wanamtafuta kuja kuyatolea ufafanuzi.
Miongoni mwa aliyotaja, ni pamoja na kashifa ya ununuzi wa sare za polisi; ununuzi wa hisa za mgodi wa makaa ya mawe uliyonunuliwa na Rostam Aziz, ambaye ameshatolea ufafanuzi madai hayo.
Mengine, ni uendeshaji wa bima ya afya, masuala ya utekaji, utesaji na mauaji na kudai kuwa baadhi ya watuhmiwa wanapatikana CCM na wako karibu na mtoto wa kiongozi mmoja mwandimizi nchini.
Jeshi la polisi nchini, kupitia msemaji wake, makao makuu mjini Dodoma, limeeleza kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), anamtaka Polepole kufika kwenye jeshi hilo na kutoa maelezo na ushahidi kuhusiana na tuhuma anazozitoa kupitia mitandao ya kijamii.
ZINAZOFANANA
Hatma kesi ya Lissu kujulikana Sept 22
Ubia ni msingi wa uchumi jumuishi katika maendeleo ya Taifa
Lissu agoma kuendelea na kesi hadi wafuasi wake waingie mahakamani