September 10, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yamwaga magari mapya kwa Polisi mkoani Mbeya

 

JESHI la Polisi mkoa wa Mbeya, limekabidhiwa magari saba aina ya Toyota Land Cruiser, yaliyotolewa na Serikali kwa lengo la kuongeza ufanisi katika shughuliki zake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya magari hayo, jana tarehe 9 Septemba, Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amesema magari hayo ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha ulinzi na usalama nchini kwa vitendo.

Alisema, “Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuboresha utendaji wa jeshi la Polisi. Imedhamiria kuwaona Polisi wanatimiza wajibu wao, bila shida. Na imedhamiria kuhakikisha haki inapatikana haraka.”

Amesema, hivyo basi, upatikanaji wa magari hayo utaleta mapinduzi katika kazi za kipolisi hasa kushughulikia kesi kwa weledi na kasi inayotakiwa.

“Rais Samia amedhihirisha falsafa ya ‘kazi na utu’ kwa vitendo kwa kupeleka miradi na vifaa muhimu vya kazi ikiwamo magari haya. Ni jukumu letu kuyatumia kikamilifu kwa malengo yaliyokusudiwa,” alieleza Itunda.

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema, kati ya magari hayo, matano yatasambazwa kwenye halmashauri tano za mkoa wa Mbeya kwa ajili ya matumizi ya maofisa upelelezi wa wilaya.

“Kupatikana kwa magari haya kutaimarisha kasi ya kufuatilia na kushughulikia kesi kwa weledi, jambo litakalosaidia wananchi kupata haki kwa haraka zaidi,” amefafanua Kuzaga.

About The Author

error: Content is protected !!