September 5, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Askari aliyetuhumiwa kumbaka mwanafunzi afukuwa kazi

Kamanda Richard Abwao

 

JESHI la Polisi Mkoa wa Tabora limemfukuza kazi askari wake mwenye cheo cha Koplo Gebasa G. 8265 aliyekuwa akifanya kazi kituo kidogo cha Polisi kata ya Sungwizi, tarafa ya Simbo, wilaya ya Igunga. Anaripoti Abdallah Amiri Igunga, Tabora … (endelea).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Kamishina msaidizi, Richard Abwao amethibitisha kufukuzwa kwa askari huyo.

Abwao amesema maamuzi wa kumfukuza kazi Askari huyo umekuja baada ya kufanya uchunguzi wa kina kufuatia tuhuma iliyokuwa ikimkabili ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili tukio lililotokea tarehe 22 Februali 2025.

Amesema katika tarehe hiyo majira ya saa 3:30 usiku katika uwanja wa mpira uliopo jirani na shule ya sekondari kata ya Nkinga, askari huyo alimbaka mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 16 anayesoma shule hiyo.

Amesema baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa hiyo walimkamata askari huyo kisha kumuweka mahabusu ambapo uchunguzi ulifanyika kwa kina na  kubaini askari huyo alishindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi na badala yake alijihusisha na kitendo hicho cha kubaka.

Kamanda Abwao alisema; “Mimi kama kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, nimefanya hivyo ikiwa ni moja ya majukumu yangu ya kusimamia nidhamu ya askari wote.

“Napenda kutoa onyo kali kwa askari yoyote atakaye bainika kufanya upuuzi kama huo  hatutasita kumfukuza kazi huku akitoa onyo pia kwa baadhi ya wananchi wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwa kuwa watakaobainika nao watakamatwa na kufikishwa mahakamani.”

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kata ya Sungwizi na Nkinga Ramadhani Juma, Adija Mussa, Issa Shabani, Rehema Sudi, kwa nyakati tofauti wamemshukuru kamanda Abwao kwa hatua aliyochukua ya kumfukuza kazi askari huyo.

Aidha wananchi hao waliomba askari huyo afikishwe mahakamani na sio kufukuzwa kazi tu kwani ushahidi upo wa kutosha. Ambapo itakuwa fundisho kwa wale wote wenye kukatiza ndoto za wanafunzi kuendelea na elimu.

About The Author

error: Content is protected !!