
ASKARI wa Idara ya Wanyamapori mkoani Mwanza, Enock Rugaimukamu Gration (33), amepoteza maisha baada ya kushambuliwa na chui wakati wa oparesheni ya kudhibiti mnyama huyo aliyekuwa ametishia usalama wa wakazi katika mtaa wa Lyago, kata ya Mahina, wilayani Nyamagana. Anaripoti Zakia Nanga, Mwanza … (endelea).
Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa tarehe 2 Septemba 2025.
Amesema tukio la awali lilitokea tarehe 29 Agosti 2025 majira ya saa 7:00 mchana, ambapo chui huyo alimjeruhi mwanafunzi wa darasa la kwanza, Juma Marwa Mniko (10) wa Shule ya Msingi Mahina, pamoja na Mshangi Mkama Msiba (45), mkulima na mkazi wa eneo hilo.
Baada ya tukio hilo, kikosi cha askari wa wanyamapori kilianza msako na tarehe 30 Agosti 2025 saa 7:30 mchana walifanikiwa kubaini maficho ya mnyama huyo katika pango. Hata hivyo, juhudi za kumdhibiti zilishindikana baada ya chui huyo kushambulia ghafla na kuwajeruhi askari watatu.
Majeruhi walihamishwa haraka kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando, lakini kwa bahati mbaya Rugaimukamu alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa kwa matibabu.
Kamanda Mutafungwa alieleza kuwa oparesheni za kudhibiti wanyama wakali na waharibifu zitaendelea kwa kushirikiana na wananchi ili kulinda maisha ya watu pamoja na mali zao.
ZINAZOFANANA
Watakaosalimisha silaha haramu kusamehewa
Mwendokasi Mbagala bado kuzungumkuti
Mambo matano ya Mwabukusi aliyomwambia Rais Samia