August 28, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Pigo jingine ACT- Wazalendo lanukia

Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo

 

MAKUMI ya wagombea wa chama cha ACT-Wazalendo, waliojiunga na chama hicho, miezi miwili iliyopita, wako hatarini kuenguliwa. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Taatifa mikononi mwa MwanaHALISI Online zinasema, karibu wagombea wote wa chama hicho, waliojiunga na ACT-Wazalendo, katika siku za karibuni, kuna uwezekano mkubwa wa kuzuiwa kushiriki uchaguzi huo.

Kuenguliwa kwa wagombea hao, kunatokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi, kumzua Luhaga Mpina, kushiriki kinyang’anyiro cha urais wa Muungano.

Katika uamuzi wake, Mutungi alisema, Mpina hakutimiza vigezo vya uanachama kwa mujibu wa kanuni za chama hicho.

Alisema, mwanasiasa huyo, alijiunga ACT-Wazalendo, nje ya muda uliopangwa na hivyo hakustahili kuwania nafasi ya urais kwa tiketi ya chama hicho.

Alitoa uamuzi huo, kufuatia pingamizi lililowasilishwa na mwanachama wa chama hicho, Monalisa Ndala.

Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za ACT-Wazalendo, mwanachama anayetaka kugombea uongozi, anapaswa kuwa amejiunga na chama hicho, siku saba kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza.

Wagombea wengi wa ACT-Wazalendo, wakiwamo wale waliotoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walijiunga na chama hicho, baada ya mchakato huo kufungwa.

MwanaHALISI Online imeelezwa kuwa baadhi ya wagombea wa chama tawala wanaokabiliana na wagombea wa ACT- Wazalendo, kuanzia ngazi ya ubunge, ujumbe wa baraza la wawakilishi na udiwani, wamejiandaa kuwawekea pingamizi kutaka waenguliwe.

Moja ya pingamizi ambalo mtandao huu umefanikiwa kuliona, ni lile lililoandikwa na Esther Matiko, anayegombea ubunge katika jimbo la Tarime Mjini (CCM).

Anapinga kuteuliwa kwa Kangoye Jackson Ryoba, aliyepitishwa kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Gazeti hili limeshundwa kuwapata viongozi wa ACT-Wazalendo, kuzungumzia suala la lini ulikuwa ukomo kwa wagombea ubunge na udiwani.

About The Author

error: Content is protected !!