August 23, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

ACT-Wazalendo wamjibu Polepole

Othman Masoud Othman

 

MWENYEKITI wa chama cha ACT-Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman (OMO), amesema chama chao si mradi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kudhoofisha siasa za upinzani kama wanavyodai baadhi ya watu. Anaripoti Salehe Mohamed, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema yeye na wenzake waliokuwa Chama cha Wananchi (CUF), kabla ya kujiunga na chama hicho walifanya uchunguzi na utafiti wa kina na kujiridhisha kuwa ACT-Wazalendo ndilo jukwaa sahihi la kufanya siasa za kizalendo za kuwapigania na kuwaunganisha Watanzania.

Othman ametoa kauli hiyo leo, tarehe 23 Agosti 2025, wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari juu ya masuala mbalimbali ya nchi ambapo amesema alichokisema aliyekuwa balozi wa Tanzania Humphrey Polepole kuwa ACT-Wazalendo ni mradi wa CCM ni propaganda zenye lengo la kuwashushia heshima mbele ya jamii.

“Baadhi yetu tuliondoka CUF kwa sababu ya serikali ya CCM na mahakama zilitufanyia uonevu na dhuluma kwa kutubagaza, tukajiunga na ACT-Wazalendo ili tupambane na chama tawala. Haiingii akilini tuondoke CUF kwa kukataa dhuluma ya CCM halafu tuje kwenye chama kinachotumika na mbaya wetu kudhoofisha upinzani”

“Anachokisema Polepole ni propaganda zisizofaa kupewa nafasi na Watanzania. Kinachotusikitisha ni kuona hata wapinzani wenzetu tuliopaswa kushirikiana kujenga upinzani imara nao wametumbukia kwenye kutudhoofisha na kutaka tutoke ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kule Zanzibar. Sisi si mradi wa CCM” amesema Othman.

Katika mkutano huo, Othman ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar, amesema hakuna kifungu cha katiba ya chama au kanuni kilichokiukwa kwenye mchakato wa kumpitisha mgombea urais wa Tanzania Bara,

Luhaga Mpina aliyejiunga na chama hicho tarehe 5 Agosti, siku iliyofuata akachukua fomu ya kuwania urais na tarehe 7 Agosti, 2025 alipitishwa na Mkutano Mkuu, kugombea urais.

“Katiba na kanuni zetu ziko wazi kabisa, tena kwenye kikao kilichompitisha Mpina ndugu yetu Monalisa Ndala aliyekwenda kupeleka malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kupinga uteuzi huo, alikuwapo na alishangilia mno kiasi kwamba watu wetu wa protokali wa mgombea walilazimika kuingilia kati. Pia kama alikuwa na hoja au maoni alipaswa ayatoe baada ya saa 48.

“Hakufanya hivyo ameibuka baada ya siku sita, tutaeleweshana tu ndiyo maana ya demokrasia na sisi ndiyo watetezi wake, nyie wote mnajua yanayoendelea lakini nawaahidi chama kitatoa taarifa vizuri maana leo hii Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Addo Shaibu alikuwa awe hapa lakini ameitwa ofisi ya msajili pamoja na mlalamikaji ili wasikilizwe. Hii ndiyo siasa hasa unapotaka kuwaondoa watawala madarakani” amesema

Mgombea huyo pia amesema kuwa wakipewa ridhaa ya kuingia madarakani katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba mwaka huu, watawaonyesha Watanzania na CCM maana ya uchaguzi huru na haki kwenye uchaguzi wa 2030.

Amesema licha ya Katiba ya mwaka 2010 kuanzisha SUK lakini wenzao (CCM) hawawapi ushirikiano unaotakiwa na pia wamekuwa wakifanya mizengwe mingi ili kuvuruga uchaguzi ujao.

“Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mbaya pengine kuliko hata ule wa 2020, kuna watu wameondolewa kwenye daftari la kudumu la kupigakura kinyume cha Katiba. Kura za mapema tulikubaliana zisiwepo lakini wenzetu wanaendelea nayo kwa kuwa wanataka washinde kwa hila. Tunakoelekea si kuzuri hata kidogo kwa kuwa wananchi wameamka huku watawala wanataka waendeleze wizi wa kura” amesema

Othman pia amewataka wananchi wabebe jukumu la kulinda kura na demokrasia badala ya kuliacha jukumu hilo kwa vyama vya siasa kama inavyofanyika hivi sasa.

“Wananchi ni wengi kuliko hao wanaoshiriki kuiba kura, kama wakiwa na uelewa na kusimamia kile walichokichagua tutakomesha wizi wa kura, tatizo lililopo nchini kwetu kudhani kazi ya kulinda kura ni ya chama fulani, sisi tumeshatoa elimu katika maeneo mengi juu ya thamani ya kura na nini maana ya kulinda demokrasia” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!