
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetunukiwa tuzo ya Benki Bora ya Kidijitali kwa Wateja Tanzania – (Tanzania’s Best Digital Bank for Consumers) kwa mwaka 2025 katika tuzo za Euromoney zilizofanyika hivi karibuni nchini Uingereza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hatua hiyo inatajwa kuwa ni uthibitisho wa umadhubuti wa jitihada za benki hiyo katika kuendesha mabadiliko ya kidijitali kwa misingi ya ubunifu, usalama, na ujumuishaji wa kifedha kwa wote.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio hayo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na Wakubwa wa benki ya NBC Bw Elibariki Masuke, aliemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema mafanikio hayo yamechagizwa na jitihada za benki hiyo katika kupambania ujumuishi wa kifedha kwa vitendo hususani kupitia maboresho makubwa ya huduma yake ya kibenki kwa njia kidigitali ya ‘NBC Kiganjani’.
“Kupitia NBC Kiganjani, tumefungua milango ya huduma za kifedha kwa Watanzania wote – mijini na vijijini, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wenye simu janja na zile za kawaida. Huduma kupitia USSD na App ni sehemu ya dhamira yetu ya kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki katika uchumi rasmi.’’ alisema.
Aidha Masuke alitaja vigezo vingine vilivyochochea mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ubunifu wa huduma za kidigitali zinazozingatia mahitaji halisi ya maisha ya kila siku ya watanzania ikiwemo malipo ya Ankara mbalimbali, uhamishaji wa fedha, mikopo midogo ya papo kwa papo, ununuzi wa tiketi za usafiri na vingamuzi.
“Zaidi watoa tuzo hii wametambua jitihada zetu kama benki katika kuendeleza miundombinu ya kidijitali ambapo kwa kutumia teknolojia ya uthibitisho kupitia NIDA, alama za vidole, na hatua mbili za uthibitisho (Two times verication), tumejenga mfumo salama, unaowezesha wateja kujiunga kwa haraka bila kuhangaika – tukichangia pia katika Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan SDG namba 9.’’
“Pia ushirikiano na wazawa kupitia Fintech imekuwa ni namna bora zaidi iliyowavutia watoa hizi kutokana na ukweli kwamba huduma nyingi ndani ya NBC Kiganjani ni matokeo ya ushirikiano na watoa huduma wa ndani yaani Fintechs zenye suluhisho za Kitanzania kwa changamoto za Kitanzania. Huu ni ushahidi wa jinsi teknolojia ya ndani inavyoweza kuendesha maendeleo ya kweli ya kuzalisha ajira kwa vijana wetu,’’ aliongeza Masuke.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa benki ya NBC, David Raymond alisema yanaakisi uhalisia wa kimasoko ambapo kwasasa benki hiyo inashuhudia ongezeko kubwa la watumiaji wa huduma za kibenki kwa njia ya kidigitali ambapo kwa sasa zaidi ya asilimia 70 ya miamala yote ya NBC inafanyika nje ya matawi ya benki hiyo huku ikishuhudiwa ukuaji wa watumiaji wa kidijitali kwa asilimia 160, ishara inayothibitisha utayari wa watanzania katika kupokea Uchumi wa kidigitali.
“Huduma kama vile ‘NBC Wakala Pesa’ imekuwa chachu ya kuhamasisha watanzania wengi kugeukia huduma za kibenki kutokana na ukweli kwamba pamoja na kurahisisha mud awa wao kufanya miamala pia haiusishi gharama yoyote katika kutuma na kupokea fedha,’’ aliongeza.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kidigitali wa benki hiyo Ulrik Peter alisema benki hiyo itaendeleza ushirikiano wake na watoa huduma wa ndani (Fintechs) ili kufanya tafiti na kubuni huduma mbalimbali za kidigitali zinazowalenga na kuwagusa watanzania kwa kuzingatia mahitaji yao halisi katika huduma za kifedha.
“Ni kwa kushirikiana na watoa huduma wa ndani (Fintechs) ndio haswa tunaweza kubuni huduma sahihi za kibenki zinazoendana huduma zetu mbalimbali zikiwemo za kijamii kama vile mashule, Hospitali na hata huduma za kibiashara,’’ alisema.
ZINAZOFANANA
Shindano jipya kutoka Meridianbet, karibu ulimwengu wa Zombie Apocalypse
Meridianbet watangaza ujio wa Imoon, mtoa huduma mpya
TRA, NCAA, TANAPA na TAWA kuunda kamati ya pamoja kuongeza mapato