July 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wanaosifia dawa za kulevya kuchukuliwa hatua kali – DCEA

 

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetoa onyo kali kwa watu wote wanaotangaza, kusifia au kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya kwa namna yoyote ile, iwe kupitia mavazi, muziki au mitandao ya kijamii ikisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kama wahalifu wengine wa dawa hizo haramu. Anaripoti Mwandisi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza leo Julai 5, 2025 katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo amesema sheria ipo wazi, na kifungu cha 24 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kinatoa mamlaka ya kuwachukulia hatua wote wanaoeneza au kuhamasisha matumizi ya dawa hizo.

Amesisitiza watakaoendelea kukaidi maelekezo ya Serikali watahakikisha hatua za kisheria zinachukua mkondo wake na wataendelea kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Mavazi, nyimbo au hata ujumbe wa kwenye mitandao vinavyohamasisha matumizi ya dawa za kulevya ni kosa kisheria. Sheria itachukua mkondo wake,” amesema Kamishna Lyimo na kuongeza kuwa Mamlaka haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wote wanaoendeleza aina yoyote ya uhamasishaji wa matumizi hayo.

Katika hatua nyingine, Kamishna Lyimo ametumia fursa hiyo kutoa ujumbe mzito kwa wale wote wanaoendelea kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini, akisema kuwa “mkono wa chuma utawafikia na sheria haitasita kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.”

Amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza upatikanaji wa dawa aina ya heroin na cocaine nchini, operesheni kabambe bado zinaendelea, kwa ushirikiano na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kuhakikisha tatizo hilo linakomeshwa kabisa.

“Leo hii, ukipita maeneo kama stendi za mabasi na mitaani, si rahisi tena kuwaona waraibu waliokuwa wakining’inia kama zamani. Hii ni kwa sababu Serikali imewaingiza kwenye mpango maalum wa tiba, na wengi wao wanapata matibabu bila malipo na wanarejea katika maisha ya kawaida,” amesema Kamishna huyo.

Ameongeza kuwa Mamlaka imeanza kampeni maalum ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kuhusu madhara ya dawa za kulevya, pamoja na kueleza bayana adhabu zinazotolewa kwa wanaokutwa na dawa hizo.

“Lengo letu si kuwakamata watu tu, bali kuelimisha jamii. Tunataka kila Mtanzania afahamu madhara ya dawa za kulevya na pia kujua kuwa Serikali ipo tayari kuwasaidia waliokwishaathirika ili warudi katika hali nzuri na kushiriki katika kujenga uchumi wa taifa,” amesema.

Aidha, Kamishna Lyimo ametoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuhakikisha wanawalinda watoto wao dhidi ya mitego ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa jukumu la kulinda kizazi kijacho ni la kila mmoja.

About The Author

error: Content is protected !!