
Prof. Kitila Mkumbo
MBUNGE wa jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo aliyemaliza muda wake, leo tarehe 30 Juni 2025, amerejesha leo fomu ya kuomba ridhaa ya kutetea kiti chake kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … ( endelea).
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hiyo, Mkumbo amesema kuwa uamuzi wake umetokana na hamasa ya kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata nane za jimbo hilo.
Ameitaja miradi hiyo ni ujenzi wa barabara, kudhibiti mito inayosababisha mafuriko na kukuza fursa za biashara kwa wakazi wa Ubungo.
“Sababu kubwa ni kwamba kazi iendelee, lakini safari hii ni katika muktadha wa ‘kazi na utu, tunasonga mbele’. Kazi kubwa ya kwenda kuifanya ni katika ujenzi wa barabara zinazopita mitaani na kushughulikia mito ya wananchi wetu kama mto China na mto Gide,” amesema Mkumbo.
Amesisitiza kuwa jimbo la Ubungo lina shughuli nyingi za kibiashara hivyo kipaumbele chake kikuu ni kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.
“Tunatarajia kuzindua mradi mkubwa sana wa uwekezaji pale Ubungo utakaosaidia kutoa ajira nyingi kwa vijana na akina mama wa eneo letu,” ameongeza Mkumbo
Mkumbo pia amesema kuwa miradi ya huduma za kijamii (elimu, afya na maji) itaendelea kupewa uzito mkubwa, huku akiahidi kushirikiana na wanachama wa CCM kuendeleza kazi ya kutatua changamoto zilizobaki.
“CCM ni chama cha kidemokrasia. Kila mwanachama ana haki ya kugombea kama ambavyo mimi nina haki. Hatimaye chama kitafanya mchujo na wanachama wataamua nani anafaa kupeperusha bendera ya chama katika Jimbo la Ubungo,” amesema.
ZINAZOFANANA
ACT kutinga mahakamani kisa kufungwa kwa mitandoa ya kijamii
Kesi dhidi ya Chadema yapigwa kalenda
Janeth Rithe aachiwa kwa dhamana