
MDHAMINI Mkuu wa ligi ya NBC, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) jana ilikabidhi kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya soka ya NBC (NBC Premier League) kwa timu ya Yanga SC ya jijini Dar es Salaam iliyoibuka bingwa wa kombe hilo msimu wa mwaka 2024/2025, huku ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwekeza zaidi kwenye maendeleo ya wachezaji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hafla ya kukabidhi kombe la ubingwa huo ilifanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dare es Salaam, ikihusisha mchezo wa mwisho wa ligi hiyo baina ya mabingwa hao na timu ya Simba SC ya jijini Dar es Salaam mchezo unaofahamika kama ‘Derby ya Kariakoo’.
Mchezo huo muhimu uliokuwa unaamua ubingwa wa ligi hiyo ulitamatika kwa timu ya Yanga SC kuibuka na ushindi wa goli 2-0 dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC na hivyo kutangazwa mabingwa rasmi wa ligi hiyo na hatimaye kukabidhiwa kikombe cha ubingwa kutoka kwa mdhamini huyo.
Hafla hiyo iliongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Athuman Nyamlani aliembatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, tukio lililoshuhudiwa na maelfu ya mashabiki wa soka nchini waliohudhuria mechi hiyo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Sabi pamoja na kuwapongeza mabingwa hao pamoja na vilabu vingine vyote vilivyoshiriki ligi hiyo, alionyesha kuvutiwa zaidi na kasi ya maendeleo katika mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini hususani ushindani mkubwa unaoendelea kushuhudiwa kwenye ligi hiyo kila msimu mpya.
“Tangu tuanze kudhamini Ligi Kuu ya NBC, tumeshuhudia ushindani mkubwa na wa kuvutia kati ya vilabu vyote vinavyoshiriki. Ushindani huu siyo tu umepandisha kiwango cha mchezo, bali pia umetufanya tushuhudie matukio ya kusisimua na burudani ya hali ya juu. Ni dhahiri kwamba kila timu inajitahidi kuonyesha uwezo wake wa hali ya juu, na hili ni jambo la kufurahisha sana kwetu kama wadhamini.’’
“Tunapofunga mwaka huu wa mashindano, tunatambua kwamba ushindani ni sehemu muhimu ya maendeleo ya michezo, na tunajivunia kuwa sehemu ya safari hii. Napenda kuwahakikishia wapenzi wa mchezo huu kuwa Benki ya NBC itaendelea kuboresha udhamini wa Ligi Kuu ya NBC msimu ujao. Tunatambua umuhimu wa kuleta mabadiliko chanya, na hivyo tumejizatiti kubuni fursa mbalimbali kwa wadau wa ligi hii,’ alisema.
Sabi alitaja baadhi ya jitihada zinazohitaji kipaumbele kuwa ni pamoja na uwezeshaji kwenye michakato ya mafunzo na maendeleo ya wachezaji hususani kwenye programu za vijana, huduma bora za bima husasani ya afya kwa wachezaji, pamoja na huduma mbalimbali za kibenki mahususi kwa wanamichezo ili kuwakwamua zaidi kiuchumi kupitia usaidizi wa kifedha na usimamizi bora hatua itakayowasaidia kufikia malengo yao ya kitaaluma na maendeleo binafsi.
Katika kutumia vema mchezo huo benki hiyo pia iliandaa usafiri maalum kwa maofisa wake na baadhi ya wateja wake jijini Dar es Salaam kwenda kushuhudia mchezo huo uwanjani sambamba na kuandaa sehemu maalum za kutazama mechi hiyo kupitia ‘screens’ kubwa kwenye baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam na baadhi ya mikoa huku pia timu ya masoko ya benki hiyo ikiwa imejipanga kutoa huduma mbalimbali za kibenki kwenye maeneo hayo pamoja na viunga vya uwanja wa Benjamin Mkapa.
ZINAZOFANANA
Meridianbet yaigusa hospitali ya Palestina Sinza
Yanga yaifikia rekodi ya Simba, yatwaa Ubingwa wa nne mfululizo
Tajirikia leo na mashindano ya Wazdan