June 24, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Simba wagomea ‘Press Conference’ kuelekea ‘Derby’

 

KLABU ya Simba imeshindwa kutokea kwenye mkutano wa waandishi wa Habari kuelekea kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwenye mkutano huo ambao upande wa Simba walipaswa kuwepo Kocha mkuu pamoja na mchezaji mmoja, kuelezea maandalizi yao kiufundi kuelekea mchezo huo.

Akithibitisha jambo hilo, Afisa Habari wa Bodi ya Ligi Kareem Boimanda, alisema kuwa wamejitahidi kuwasiliana na uongozi wa klabu hiyo, ili kujua kama kuna changamoto yoyote lakini walishindwa kuwapata.

“Tumewakosa Simba ili watueleze changamoto yoyote wamekutana nayo wakati wakiwa njiani, tunaendelea kuwatafuta tutakapojua nini changamoto tutawajuza.” Alisema Boimanda

Mkutano huo ulipangwa kufanyika majira ya saa 5:30, ambapo hapo awali ulitanguliwa na mkutano wa klabu ya Yanga uliofanyika majira ya saa 5 kamili.

Mchezo huo namba 184, ambao ulipangwa na kuahirishwa mara kadhaa, utapigwa kwenye kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, majira ya saa 11 jioni, ukiwa ni mchezo wa mwisho kukamilisha msimu wa 2024/25.

Kupitia mchezo huo, bingwa rasmi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, atafahamika kufuatia timu hizo kupishana alama moja tu, ambapo Yanga mpaka sasa wanapointi 79, huku Simba wakiwa na pointi 78.

Ili Yanga kutetea ubingwa wao kwenye mchezo huo, wanahitaji ushindi au sare ya aina yoyote, huku Simba wao wakihitaji matokeo ya ushindi tu.

About The Author

error: Content is protected !!