May 21, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mvunde aongoza kikao cha kimkakati wa kiuchumi kupitia STAMICO

Anthony Mavunde, Waziri wa Madini

SHIRIKA la  Madini la Taifa  (STAMICO) limekaa Mguu Sawa kuhamia kwenye Uwekezaji Mkubwa wa  Madini Muhimu na Madini Mkakati huku tayari likiwa na mafanikio kadhaa ikiwemo kuachana na utegemezi kwa Serikali kwa asilimia 100 na likiwa limekwisha toa gawio kwa Serikali  ya kiasi cha Sh. 9 bilioni. Anaripoti Joyce Ndeki, Dodoma … (endelea).

Hayo  yalibainishwa Mei 19, 2025 zikiwa zimepita siku kadhaa tangu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lipitishe Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 ambapo miongoni mwa yaliyopangwa kutekelezwa mwaka ujao ni pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini muhimu na mkakati.

Mbali na hayo, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Shirika hilo linakua kubwa kama ilivyo malengo ya kuanzishwa kwake ya kuwekeza kwa niaba ya Serikali ambapo miongoni mwa majukumu yake ni pamoja na kuwekeza  kwenye miradi ya kimkakati ya utafutaji na uchimbaji madini  ili kuongeza manufaa zaidi kwa taifa.

Kikao hicho ni cha pili baada ya kikao cha kwanza kilichofanyika Mei 12, 2025 jijini Dodoma ambavyo vyote vimeongozwa na Anthony Mavunde Waziri wa Madini  vikihusisha Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake ili kujadili kwa pamoja andiko la kuiwezesha STAMICO) kuwekeza katika uchimbaji mkubwa wa madini nchini.

Awali, STAMICO liliwekwa kwenye orodha ya mashirika yanayopaswa kufutwa na Serikali  na miaka ya karibuni, kupitia Falsafa ya 4 Rs za Samia Suluhu Hassan Rais wa Awamu ya sita, Shirika lineweza kuishi mageuzi jayo kwa vitendo na kuweza kuwa miongozi mwa mashirika ya mfano yanayofanya vizuri na sasa  limejikita kuwekeza katika shughuli za uchimbaji mkubwa na wa Kati wa madini muhimu na mkakati pamoja na dhahabu katika zama hizi  ambazo mataifa mengi duniani yanapambana  kuhakikisha yananufaika na rasilimali madini zilizopo kwenye nchi zao.

Akizungumza katika kikao hicho, Mavunde amesema miradi inayotarajiwa kufanywa na STAMICO italirejesha tena shirika hilo kwenye ramani ya dunia na kusisitiza kwamba, matamanio yake ni kuliona  shirika  hilo linakua  kubwa kama ilivyo kwa Kampuni kubwa kama  Barrick Gold Mine na AngloGold Ashanti  ili liweze kuongeza manufaa zaidi kwa  nchi kupitia rasilimali madini zinazopatikana nchini.

‘’ Ninawapongeza STAMICO kwa hatua kubwa mliyopiga hadi mlipo sasa. Miradi hii pindi itakapotekelezwa, kama taifa tutakwenda kunufaika ipasavyo na kusema, ‘’tukipata nafasi ya kuifanya kazi wenyewe, manufaa yake ni makubwa.

Shirika hili ni muhimu sana katika kuisaidia nchi yetu kunufaika na rasilimali madini,tutatumia maarifa na ujuzi wote kuhakikisha STAMICO inakuwa moja kati ya mashirika makubwa ya umma katika kushiriki kikamilifu kwenye sekta ya madini barani Afrika kwa kuja na kauli mbiu ya  MASTASHA (𝙈𝙖𝙠𝙚 𝙎𝙏𝘼𝙈𝙄𝘾𝙊 𝙎𝙝𝙞𝙣𝙚 𝘼𝙜𝙖𝙞𝙣)kulirudishia ari,nguvu na malengo iliyokuwa nayo wakati  wa uanzishwaji wake’’ amesema Waziri Mavunde.

Akizungumza katika kikao hicho, Venance Mwasse Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO amekielekeza kikao hicho kuhusu mipango kabambe iliyopangwa kutekelezwa na shirika hilo, pamoja na kueleza manufaa ya miradi hiyo ikiwemo kutoa ajira za moja kwa moja, mapato kwa serikali, kuongeza ushindani na  uwekezaji kutoka nje  kwa lenfo la kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya teknolojia.

About The Author

error: Content is protected !!