May 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mawaziri Ghana mtegoni, watishia kufutwa kazi

John Mahama

 

JOHN Mahama, Rais wa Ghana amewaonya mawaziri na wateule wengine zaidi ya 40 wa serikali yake kuwa watafutwa kazi ikiwa watashindwa kuweka wazi mali wanazomiliki ifikapo kesho Jumatano ya tarehe 7 Mei, ambayo ndiyo siku ya mwisho iliyowekwa kwa ajili ya zoezi hilo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Tangu alipoapishwa kuwa rais mwezi Januari, Mahama ameahidi kupambana na ufisadi wakati akijaribu kuimarisha uchumi wa nchi hiyo.

Akihutubia hadhara siku ya Jumatatu, Rais wa Ghana alisema, wale watakaobainika kwenda kinyume na tarehe ya mwisho ya kuweka wazi mali wanazomiliki kufikia Jumatano, ambayo awali ilikuwa 31 Machi, hawatopokea mshahara wa miezi minne – mitatu kama adhabu na wa mwezi mmoja kuchangia kwa lazima mradi wa mfuko mpya wa kusaidia masuala ya matibabu, maarufu nchini Ghana kama “Mahama Cares”.

“Kama kufikia mwisho wa siku ya Jumatano, 7 Mei, 2025, yeyote kati yenu atakuwa hajaweka wazi mali anazomiliki, fahamu mara moja kuwa umeshafutwa kazi”, alisisitiza kiongozi huyo.

Katika hotuba yake hiyo, Mahama aliahidi kuwa onyo hilo si la mzaha na litatekelezwa. Na akaongezea kwa kusema: “sitosita kuchukua hatua kali na madhubuti, bila kujali nani anahusika.”

Kanuni mpya za maadili zilizowekwa na serikali mpya ya Mahama ni kwa wateule wote wa kisiasa, wakiwemo mawaziri, manaibu waziri, wafanyakazi wa ofisi ya rais na Rais mwenyewe.

Watetezi wa masuala ya utawala bora wameipongeza hatua hiyo kama jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Ghana.

Emmanuel Wilson Jr, mwanaharakati wa kupinga ufisadi wa shirika la ‘Crusaders Against Corruption’ amesema: “hili ni jambo la kimaadili na kiutekelezaji kuwahi kutangazwa na rais wa Ghana aliyeko madarakani”.

About The Author

error: Content is protected !!