May 4, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

EXIM yatangaza mafanikio makubwa na mwelekeo madhubuti 2025

BENKI ya Exim Tanzania imeanza mwaka kwa mafanikio makubwa, baada ya kuhitimisha robo ya kwanza ya mwaka 2025 kwa matokeo chanya yanayoonesha kasi ya ukuaji, ufanisi wa utendaji na jitihada madhubuti zinazolenga ubunifu na ujumuishaji wa huduma za kifedha kwa wote. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa kipindi kilichoishia Machi 2025, benki ya Exim imetoa takwimu thabiti za kifedha ambazo zinaendelea kuimarisha nafasi yake kama benki inayoongoza sekta binafsi nchini.

Mapato ya benki yameongezeka na kufikia Sh. 3.4 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. Mikopo waliyokopeshwa wateja imeongezeka hadi Sh. 1.9 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 20. Hii inaonesha namna ambavyo benki inaendelea kusaidia watu binafsi na biashara katika sekta mbalimbali za uchumi.

Faida kabla ya kodi kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025 ilikuwa Sh. 26.5 bilioni, mafanikio yanayoonyesha utekelezaji mzuri wa mikakati ya benki ya Exim, ikiwemo kuzingatia mahitaji ya wateja, usimamizi makini wa mikopo, na kuwekeza katika huduma bunifu zinazowafikia Watanzania wengi zaidi.

Amana za wateja zimeongezeka na kufikia Sh. 2.7 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 20 ukilinganisha na mwaka uliopita, jambo linalodhihirisha imani kubwa ya wateja kwa huduma zinazotolewa na benki ya Exim. Mapato kutoka riba kwa kipindi hicho yalifikia Sh. 43.7 bilioni, ongezeko la asilimia 7 kutokana na maboresho katika ubora wa mali na mikakati bora ya utoaji mikopo.

Akizungumzia matokeo haya, Afisa Mkuu wa Fedha wa benki ya Exim, Shani Kinswaga alisema “Tumeridhishwa na matokeo ya robo ya kwanza ya mwaka huu, si tu kwa sababu ya ongezeko la mapato, bali pia kwa kuwa yanaonyesha athari nzuri ya kazi zetu katika kufikisha huduma jumuishi na bunifu kwa wateja. Tutaendelea kutoa huduma rahisi, za kisasa, na rafiki kwa mteja zinazochochea maendeleo ya kiuchumi kwa Watanzania.”

Katika kipindi hiki, benki ya Exim pia ilikamilisha ununuzi wa mali na madeni ya Canara Bank Tanzania Limited, ikiwa ni mara ya tatu kwa benki ya Exim kufanya ununuzi wa taasisi nyingine ndani ya miaka sita. Hatua hii imeendelea kuimarisha nafasi ya benki ya Exim kwenye soko la Tanzania.

Kwa upande mwingine, benki ya Exim imeboresha huduma ya Mikopo kwa Watumishi wa Umma, maarufu kama Wafanyakazi Loan, ili kuwawezesha kupata mikopo kwa haraka, kwa gharama nafuu na masharti nafuu zaidi. Exim imekuwa taasisi ya kwanza nchini kutoa huduma ya kuhamisha mikopo ya watumishi wa umma kutoka benki nyingine kupitia mfumo wa kidijitali wa Employee Self Service (ESS). Huduma hii inalenga kurahisisha upatikanaji wa mikopo bora kwa watumishi wa umma, kwa urahisi na haraka zaidi.

Exim Bank inaendelea kuhimiza wateja wake kutumia huduma za kidijitali kama vile Exim Mobile na Internet Banking, ambazo zinamwezesha mteja kufanya miamala mahali popote na wakati wowote,hatua inayolenga kujenga utamaduni wa kifedha unaoendana na teknolojia ya kisasa.

Pia, huduma ya Lipa Chapchap imendelea kushika kasi katika kipindi hiki. Hii ni huduma ya malipo ya papo kwa hapo inayowezesha wateja kufanya miamala ya bidhaa na huduma kupitia QR Code na Lipa Namba. Lipa Chap Chap inalenga kurahisisha maisha ya kila siku ya watu na biashara kwa njia ya haraka, salama na isiyo na usumbufu.

Tunapoingia katika robo ya pili ya mwaka, benki ya Exim inaendelea kuonesha dhamira yake ya kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo ya nchi. Mfano mzuri ni msaada wa madarasa uliotolewa katika Wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma, ambao ni miongoni mwa miradi ya kijamii inayolenga kuinua maisha ya Watanzania, sambamba na malengo ya maendeleo ya taifa.

Ikiwa na misingi imara kifedha na dhamira ya kuwahudumia Watanzania kwa ukaribu zaidi, benki ya Exim itaendelea kushirikiana na Serikali na jamii kwa ujumla kuhakikisha maendeleo haya yanawanufaisha wananchi wengi zaidi.

About The Author

error: Content is protected !!