
CHAMA cha ACT Wazalendo kupitia Kamati ya Uongozi ya Taifa imeamua kuwa Chama hicho kitashiriki kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa nafasi zote kwani kususia uchaguzi kutaimarisha hujuma zaidi za dola dhidi ya demokrasia kwa kutoa mwanya wa kupora kwa urahisi sauti ya wananchi. Anaripoti Apaikunda Mosha, Zanzibar … (endelea).
Hayo ameyasema leo tarehe 16 aprili 2025 Kiongozi wa chama hicho Dorothy Semu akiwa makao makuu ya Chama hicho Vuga, Zanzibar.
“Kamati ya Uongozi, kabla ya kufikia uamuzi huu ilifanya tafakuri ya kina na kujiridhisha kuwa huu ndio uamuzi sahihi unaopaswa kuchukuliwa na Chama chetu kwa kuzingatia hali halisi ya kisiasa katika nchi na wajibu wa kimapambano ambao ACT Wazalendo imeubeba,” amesema Semu.
Amesema sababu zilizowasukuma kuamua kushiriki katika Uchaguzi Mkuu 2025 ni pamoja na kutetea na Kulinda Thamani ya Kura.
Doroth amesema kuwa chama cha ACT Wazalendo kinafahamu kuwa uchaguzi sio mali ya vyama vya siasa, bali ni mali ya wananchi wenyewe. Hivyo basi, Chama hicho kwa kutambua dhima kubwa iliyoibeba, kinakusudia kuhamasisha vuguvugu kubwa la wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu 2025 kutetea na kulinda haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.
“Tupo tayari kuwaongoza Watanzania kupitia vuguvugu la wananchi kutetea thamani ya kura ili kulinda msingi wa katiba yetu kuwa madaraka yote yanatoka kwa wananchi. Tupo tayari kwa mapambano!” amesema Dorothy.
Aidha Dorothy amesisistiza kuwa kususia Uchaguzi Kunaimarisha Hujuma Dhidi ya Demokrasia hivyo chama kimejiridhisha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinahitaji na kwa hakika kitafurahia iwapo vyama makini vya upinzani vitasusia uchaguzi ili kiendeleze hujuma kwa demokrasia nchini.
Hata hivyo ameeleza kuwa chama hicho kinaenda kuutumia Uchaguzi Mkuu 2025 kama uwanja wa mapambano ya kuzuia hujuma dhidi ya demokrasia. Tunakwenda kuutumia uchaguzi kudai mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi. Kwetu, Uchaguzi Mkuu 2025 ni uwanja wa mapambano!
Kwa mujibu wa Dorothy CCM imeshindwa kuongoza nchi hivo ni fursa kwa ACT wazalendo kushinda uchaguzi amesisitiza kuwa chama cha CCM kimeshindwa kuwakomboa Watanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii, hivyo inaashiria kuwa CCM imechoka na haiwezi tena kuwa na fikra za kuwakomboa Watanzania.
Mwisho amesema kupitia ‘Operesheni ya Linda Demokrasia’ Chama kinaendelea kuunganisha nuvu za wananchi kuitetea na kuilinda demokrasia nchini, hivyo amewasihi watanzania kutokata tamaa kuipigania demokrasia ya nchi yetu.
ZINAZOFANANA
Dk. Kimei aweka rekodi ya utendaji Vunjo
Othman Masoud: Tunaingia kwenye uchaguzi mkuu Oktoba tukiamini sisi ni washindi
Othman akabidhiwa mazito ACT Wazalendo