
WAZIRI wa Nchi Ofis ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema tangu kuasisiwa na kutangazwa rasmi kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar 26 Aprili 1964, kumekuwa na mafanikio makubwa na ya kujivunia kwa Watanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Amesema hayo wakati wa Semina kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, iliyofanyika Dodoma Aprili, 2025, huku akieleza mafanikio hayo yameambatana na faida pamoja na fursa nyingi.
“Kabla ya Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar utumishi wa umma ulisimamiwa na wakoloni. Katika kipindi hicho idadi ndogo ya Watanganyika na Wazanzibari waliajiriwa kwa lengo la kulinda na kuendeleza maslahi ya wakoloni, tofauti na sasa.
Kuhusu elimu amesema, wakati wa ukoloni elimu ilitolewa kwa misingi ya kibaguzi hasa kulingana na rangi, imani na pia ushirika wa karibu wa wakoloni na malengo tofauti ya wageni au wakoloni hao.
Uwepo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni moja ya faida ya Muungano kwani, mara baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar 26/4/1964 lilianzishwa Bunge la pamoja yaani Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linalojumuisha wajumbe kutoka pande zote mbili za muungano, huku faida nyingine ni uwepo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Muungano wa Afrika na Wa-Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Juma Salum amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zina dhamira ya dhati kuhakikisha kuwa changamoto zilizopo na zitakazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano.
“Mwaka 2006 Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maagizo ya kuwataka Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kukutana na kujadili namna ya kutatua changamoto zinazoukabili Muungano wetu.
“Lengo la kuweka utaratibu huo ni kuimarisha Muungano kwa kuhakikisha kuwa, changamoto zote zinatafutiwa ufumbuzi wa kudumu. Kwa mujibu wa hoja za Muungano zilizoorodheshwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar,” alisema Dk. Salum.
Tokea kuanzishwa kwa utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano kupitia vikao hivyo mwaka 2006, hoja zipatazo 25 zimejadiliwa ambapo kati ya hizo hoja 22 zimeshapatiwa ufumbuzi.
ZINAZOFANANA
Watanzania wahimiza kufanya mazoezi kwa Afya
Ofisi ya Msajili Hazina yaendesha mafunzo kwa kamati za bunge
Puma Energy Tanzania yazindua awamu ya pili ya Kampeni ya Usalama Barabarani kwa wanafunzi wa msingi