
OFISI ya Msajili wa Hazina imeendesha mafunzo kwa Kamati tatu za Kudumu za Bunge kuhusu Mageuzi, Mafanikio, Mikakati na Mwelekeo wa Ofisi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Mafunzo hayo yaliyofanyika Ijumaa, Aprili 11, 2025, Jijini Dodoma yamehusisha Wabunge wa Kamati za Utawala, Katiba na Sheria, Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, pamoja na ile ya Bajeti.
Akifungua mafunzo hayo jana Jijini Dodoma Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Haroon Nyongo, alisema Mafunzo hayo yanalenga kujenga uelewa wa kina kuhusu Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mafunzo hayo yalijikita katika eneo la utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, mafanikio, changamoto, mikakati na uelekeo wa taasisi hiyo kuelekea mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji wa Mashirika yasiyo ya kibiashara, Dk. Emmanuel Luvanda alisema mwenendo wa ukusanyaji wa mapato yasiyokuwa ya kodi umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka.
Alisema utoaji wa gawio kutoka taasisi zinazojiendesha kibiashara, kwa wastani, umekuwa ukiongezeka kwa asilimia 50 kila mwaka.
Dk. Luvanda akizungumzia mafanikio ya Ofisi hiyo, alitaja kuboreshwa kwa taasisi na mashirika ya umma kulikochagizwa na kuongezewa mtaji, kama moja ya mafanikio ya mageuzi yanayoendelea.
Akitolea mfano wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB) iliyoongezewa mtaji wa Sh. 131 bilioni, alisema taasisi hiyo ya fedha imeongeza ufanisi wake uliopelekea kupata faida ya Sh. 31.6 bilioni mwaka 2024.
Aliendelea kusema Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liliongezewa mtaji wa kiasi cha shilingi trilioni 2.4 na hivyo kuongeza ufanisi uliopelekea kuongezeka kwa faida kutoka Sh. 8.9 bilioni hadi kufikia bilioni 21.8 kwa mwaka 2024.
Kwa upande mwingine, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) lililoongezewa shilingi trilioni 2.7, faida yake ilipanda kutoka Sh. 159.6 bilioni hadi kufikia Sh. 306 billioni mwaka 2023/24.
Mafanikio mengine aliyowasilisha Dk. Luvanda ni pamoja na Taasisi 57 za kibiashara na za kimkakati kupewa Uhuru wa kujiendesha ili kufikia ufanisi uliotarajiwa wakati wa uanzishwaji wake.
Kwa upande wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache (Minority Interest Companies), alisema tija kubwa imepatikana ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa marejeo ya mikataba ya wanahisa, kuhakikisha yanaakisi mabadiliko ya soko na kuendeshwa kwa majadiliano na wabia wenza.
Hatua hiyo imeleta mabadiliko chanya kimuundo na kiuendeshaji wa Kampuni hizo.
Mikataba hiyo ni Pamoja na ile ya Mbeya Cement, unaohusu mabadiliko ya uendeshaji wa Kiwanda cha Saruji Mbeya; Mkataba uliorejewa wa wanahisa wa benki ya NMB baina ya Msajili wa Hazina na Arise BV, na makubaliano ya kununua hisa katika Kampuni ya IDTL (asilimia 25),
Pia Ofisi ya Msajili wa Hazina imefanya makubaliano na Inflight Catering Services kuhusu kuongeza asilimia 10.99 ya hisa za Serikali kufikia asilimia 31.69 na makubaliano na Persus Mining kuhusu kuongeza hisa za Serikali katika Kampuni ya Sotta Mining kutoka asilimia 16 hadi 20 za sasa.
Akizungumzia vipaumbele vya Ofisi hiyo kwasasa, Dk. Luvanda alisema Ofisi inajielekeza katika kufanya tathmini ya mali zilizorejeshwa, tathmini ya utendaji wa Mashirika na Taasisi zilizobinafsishwa, kuongeza ufanisi wa uwekezaji wa taasisi na Mashirika ya Umma yanayolenga kuboresha huduma na kuongeza Mapato yasiyo ya kikodi, na kuboresha mifumo ya TEHAMA.
ZINAZOFANANA
Watanzania wahimiza kufanya mazoezi kwa Afya
Waziri Masauni aelezea mafanikio ya Muungano
Puma Energy Tanzania yazindua awamu ya pili ya Kampeni ya Usalama Barabarani kwa wanafunzi wa msingi