
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi zimewezesha kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 8,458 mwaka 2020 hadi kufika 9,826 Februari, 2025. Anaripoti Apaikunda Mosha. Dodoma … (endelea).
Amesema hayo leo tarehe 9 Aprili, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akitoa hotuba yake ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2025/2026.
Majaliwa amesema Sh. 74.85 bilioni zimetolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati 7, vituo vya afya 41 na hospitali 89 za halmashauri ambazo zitasaidia kusogeza huduma za afya ya msingi karibu na wananchi na hivyo kuwapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Vilevile serikali imeendelea kuboresha na kuweka mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa utoaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya
Amebainisha “Kati ya vituo hivyo, hospitali za wilaya ni 185, vituo vya afya 836, zahanati 3,778, kliniki 7 na hospitali teule za wilaya 7, ambapo wagonjwa zaidi ya milioni sita wamepata huduma kupitia mfumo huu na rufaa 10,264 zilitolewa kwa wagonjwa. Matumizi ya mfumo huo yamesaidia kudhibiti upotevu wa dawa na vifaa tiba, kudhibiti na kuongeza makusanyo ya ada za kuchangia huduma na ubadilishanaji na utoaji wa taarifa kwa wakati.”
Pia amesema kuwa idadi ya hospitali zinazotoa huduma ya magonjwa ya dharura zimeongezeka kutoka saba mwaka 2020 hadi 116 mwaka 2025. Vilevile, vituo vya kutolea huduma za afya vyenye majengo ya mama na mtoto vimeongezeka kutoka 6,081 mwaka 2020 hadi 7,397 Februari, 2025.
Amebainisha pia kuwa huduma za kibingwa na bobezi sasa zinapatikana katika hospitali za rufaa za mikoa, zinatoa huduma za afya ya uzazi na magonjwa ya wanawake, afya ya watoto, magonjwa ya ndani, upasuaji, upasuaji mifupa, huduma za dharura, huduma za mionzi, huduma za ganzi na dawa za usingizi.
Kwa upande wa vifaa tiba na vitendanishi vya kisasa na bidhaa za afya amesema vimeimarika kutoka asilimia 73 mwaka 2020 hadi asilimia 89.3 Februari, 2025 na mafanikio hayo makubwa yameendelea kuwavutia wagonjwa kutoka nje ya nchi na kuimarisha Tiba Utalii ambapo hadi Februari, 2025 wagonjwa 7,843 kutoka nje ya nchi wametibiwa ikilinganishwa na wagonjwa 5,705 mwaka 2020.
ZINAZOFANANA
Othman akabidhiwa mazito ACT Wazalendo
Othman: Tutairudisha mamlaka yenu
Mwenyekiti wa Chadema ashitakiwa kwa Uhaini