
Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Antiphas Lissu, amesema viongozi unaowapata na namna unavyowapata ndivyo utakavyovuna matokeo ya uongozi wao hivyo tusitegemee neema kama tutachagua viongozi wa hovyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Ruvuma … (endelea).
Akihutubia leo tarehe 9 Aprili 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Lissu amesema ni muhimu kuzungumza namna ambavyo kiongozi bora anapatikana kwa sababu upatikanaji wake utaamua namna atakavyotumia madaraka aliyopewa.
“Mmefanya uchaguzi hapa mwaka jana, mlichaguaje? Wapinzani wote walienguliwa, hamkuchagua lakini wapo, walipachikwa… sasa kama hujamchagua mwenyekiti wa kijiji ukakamatwa na TANAPA hapo mwenyekiti gani anakuja kukusemea wewe?” amesema Lissu.
Lissu ameeleza kuwa chaguzi zote zilizofanyika kipindi cha nyuma hazikuwa za haki hivvyo amesisitiza kuwa kama zote zilikuwa hivyo hata sasa hakutakuwa na unafuu mpaka uwekwe utaratibu mpya wa uchaguzi.
“Hatuwezi tukapata nafuu kwa sababu mfumo wa uchaguzi umetengenezwa kuwalinda, Tume yote imeteuliwa na Samia ambae ni mgombea…Mkurugenzi ni CCM, Tume ni CCM, Mtendaji wa kata ni CCM na hao wanaosimamia huko vijijini ni CCM watupu! mnatokea wapi? tukigombea wanakata wagombea wetu wote,” amesema Lissu.
Aliendelea ..“Tunahitaji kubadilisha utaratibu wa uchaguzi ili kukiwa na uchaguzi tuwe na wagombea, na kusiwe tena na wagombea wa kupita bila kupingwa, kwa sababu wakipita bila kupingwa hampigi kura na huyo ambae hujampigia kura atakutetea wapi?”
Aidha Lissu amesisitiza yafuatayo “Moja, Hatutaki chaguzi zinazosimamiwa na CCM, pili hatutaki taratibu za uchaguzi zinazoruhusu wagombea wengine kuenguliwa wakabaki mmoja mmoja, Tatu hatutaki tena kuwepo kwa kura feki kwenye chaguzi zetu, tunahitaji kubadilisha utaratibu wote wa kuandikisha wapiga kura ili kusiwe na wapiga kura maruhani”.
Aliendelea jambo la nne na tano “tuwe na utaratibu wa kampeni usioruhusu vurugu kwa wapinzani, hatutaki tena uchaguzi usiokuwa na mawakala au ambao una mawakala wa CCM pekee yao, tunataka sheria itamke kwamba kama hakuna mawakala wa Chama kinachoshiriki uchaguzi kwenye hicho kituo usimame mpaka mawakala watakapopatikana”.
Mwisho amesema “hakuna tena uchaguzi nchi hii ambao zinasababisha watoto wetu kuuwawa au kujeruhiwa ili CCM wapate madaraka.”
ZINAZOFANANA
Othman akabidhiwa mazito ACT Wazalendo
Othman: Tutairudisha mamlaka yenu
Mwenyekiti wa Chadema ashitakiwa kwa Uhaini