
MAKAMU Mwenyekiti Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche amesema vikao vya Chama hicho vinathibitisha bila kuwa na shaka, kwa mazingira ya sasa hawawezi kushinda uchaguzi hivyo ni lazima zitumike mbinu ili uchaguzi uwe huru nawa haki. Anaripoti Mwandishi Wetu. Dar es Salaam … (endelea).
Amezungumza hayo leo tarehe 3 Aprili 2025 kwenye kikao cha watiania wa ubunge wa majimbo mbalimbali nchini kupitia CHADEMA na viongozi wa kitaifa wa chama hicho, hafla iliyofanyika makao makuu ya CHADEMA, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
Heche amesema “nchi yetu inalilia mabadiliko, watu wamefanywa maskini, rasilimali zao zinauzwa kwa Wachina, watu wanahitaji uongozi mbadala na uongozi mbadala hauwezi kupatikana kwa njia hizi, CCM hawataki uchaguzi huru kwa sababu wanajua hawawezi kushinda wakienda katika uchaguzi huru.”
Akizungumzia takwimu za uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka jana (2024) amesema wagombea zaidi ya elfu 60 waliondolewa kwenye uchaguzi huo pasipo sababu za msingi.
“Tusidanganyane, tumekaa kwenye vikao tukathibitisha kwa pamoja kwamba tukienda hivi hatuwezi kushinda uchaguzi wowote ndani ya nchi hii hivyo ni lazima mabadiliko yafanyike,” amesisitiza Heche.
Ameeleza kuwa Chaguzi zilizopita hazikuwa za haki hata hivyo baada ya uchaguzi wa mwaka 2019 na 2020 walipoenda ikulu, Rais mwenyewe alisema yaliyojitokeza 2019 na 2020 hayatajirudia tena.
Aliendelea “Tumeshiriki kikao, Mwenyekiti Mbowe anatuongoza, tulikuwa na Mnyika na Kinana alikuwa anaongoza timu ya CCM na nyaraka tunazo, ‘yaliyojitokeza hayatajitokeza tena’ hiyo ni kauli ya Kinana na ipo kwenye maandishi. Nini kilichojitokeza 2024? Tumesimamisha wagombea 88 Tarime wamekata karibia asilimia 60 kabla hatujaingia kwenye uchaguzi, vitongoji 500 wamekata asilimia 60.”
Ameongeza, “kwa mujibu wa kauli ya Waziri wa TAMISEMI iliyotolewa kwa waandishi wa habari alisema wagombea 12,600 wa upinzani wameondolewa kwa sababu ya kukosea kujaza fomu, kugonga miuri vibaya na kadhalika, maana yake tunaenda kwenye uchaguzi CCM ikiwa tayari imeshinda wagombea 12,000 na kwa mujibu wa takwimu zetu wagombea zaidi ya 60,000 wa CHADEMA waliondolewa.”
“Sasa mtu anasimama anasema sijui msipoenda kwenye uchaguzi chama kitashindwa, hii si sehemu ya biashara, kama unataka kufanya biashara kafungue duka ufanye biashara. Hii ni taasisi ya kisiasa ya mapambano na tutashinda,” amesisitiza Heche.
Amesema wananchi wanaunga chama hicho mkono na wanaunga mkono ajenda ya Hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi (No Reforms, No Election), amesema watu wanatamani kugombea lakini mazingira yaliyopo hayaruhusu kushinda uchaguzi, hivyo lazima mabadiliko yafanyike.
ZINAZOFANANA
Waziri Tabia ajilipua
Katibu wa Sekretarieti ya Chadema atoa sababu za kuenguliwa
Sheikh Ponda: Mifumo ya uchaguzi irekebishwe