April 2, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Sheikh Ponda: Mifumo ya uchaguzi irekebishwe

Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda

 

SHURA ya Maimamu Tanzania imetoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan kukutana tena na wadau wa vyama vya siasa ili kufanya marekebisho ya mifumo ya uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea),

Wito huo umetolewa leo tarehe 31 Machi 2025 na Katibu Mkuu wa Shura hiyo Sheikh Ponda Issa Ponda alipokuwa akisoma wa Waraka wa Eid katika baraza la Eid lililoandaliwa na Shura hiyo katika Msikiti wa Tungi jijini Dar es Salaam.

Sheikh Ponda amesema kuwa marekebisho hayo yanachagizwa na malalamiko ya vyaka vikuu vya upinzani Chadema Tanzania Bara na ACT Wazalendo visiwani Zanzibar.

“Kauli ya Chadema “No Reform, No election” na ile ya ACT Wazalendo ya kupinga uchaguzi wa siku mbili Zanzibar, zinaakisi malalamiko ya uchaguzi mbovu kama ule wa serikali ya mtaa 2019, Uchaguzi Mkuu 2020, na uchaguzi wa serikali za mtaa 2024,” amesema Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda amesema kuwa Shura hiyo imefuatilia kauli mbalimbali za viongozi wa serikali, wanasheria na viongozi wa dini zilikuwa zimekiri dosari za uchaguzi hizo.

“Ukiachilia mbali vyama hivyo, viongozi wa serikali, wanasheria na viongozi wa dini kwa nyakati tofauti wamekiri kwamba chaguzi hizo zilikua na kasoro kubwa mno na wengi wao wanasema kasoro hizo ni kubwa kwa kiasi cha kusema hapakuwa na uchaguzi,” amesema Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda anasema kuwa kuendelea kuvurugwa uchaguzi kunaweza kuhatarisha usalama Shura hiyo imetoa wito kwa Rais Samia kufanya marekebisho ya mifumo ya uchaguzi.

“Kwa kuwa mfumo uliotumika unapoka haki za wananchi za kidemokrasia, haki ya kuishi na kuhatarisha usalama wa taifa kwa ujumla, tuna toa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuitisha wadau wawakilisha wa umma kujadili utekelezwaji wa makubaliano ya msingi ya mfumo wa uendeshwaji wa uchaguzi yaliyofikiwa, kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025,” amesema Sheikh Ponda.

Wakati huo huo Shura hiyo imesema kuwa imeshtushwa na kauli ya Rais Samia ya kulitaka Jeshi la Wananchi (JWTZ), kujiandaa na uchaguzi.

“Tumepokea kwa mshtuko mkubwa: Tamko la Rais Samia Suluhu Hassan la kuliagiza Jeshi la Ulinzi (JWTZ), lijiandae kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025. Mshtuko wetu ni kwa kua suala la uchaguzi ni la kiraia na jeshi halihusiki na masuala ya kiraia.

“Ni kweli kwamba Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa yanatuhumiwa kwa kiasi kubwa na wananchi kupora haki zao katika chaguzi mbalimbali, lakini pamoja na hayo kwa mujibu wa Katiba ya nchi wao ndio weyenye dhamana ya kulinda uchaguzi wa kiraia,” amesema Sheikh Ponda.

Waraka huo mbali na kuwakumbusha Waislam kuishi katika maadili mema umeliomba Bunge la Tanzania kufuta sheria kandamizi hususan sheria ya ugaidi.

“Tunatoa wito kwa Bunge lizifute sheria zote kandamizi zilizomo katika mfumo wa sheria wa Taifa letu. Miongoni mwa hizo ni zile zilizotajwa na Tume ya Jaji Nyalali (1991). Sheria nyingine kandamizi ya kufutwa ni ile inayoitwa ya kupambana na Ugaidi”

Sheikh Ponda amesema kuwa Sheria hizo zimewalenga waislamu, “Sheria hii ambayo inamnyang’anya mtuhumiwa haki zake zote za msingi, inatumika kuwatuhumu na kuwakamata watu wa imani hasa Waislamu. Kiasi kwamba imejengwa dhana kwa wananchi kuwa serikali ya Tanzania ina ajenda dhidi ya Uislamu na Waislamu”

Shura hiyo imeitaka serikali kupeleka ushahidi mahakamani kwa watuhumiwa wa mashauri ya ugaidi ili wapate haki zao.

“Aidha tunaikumbusha serikali ipeleke ushahidi mahakamani ili Waislamu wakiwemo Masheikh Maimamu, Waalimu wa Madrasa, Wasomi wa vyuo vikuu na waumini wa kawaida, inaowashikilia kwa tuhuma za ugaidi wapate haki yao ya kujitetea na kusomewa hukumu.

“Tunaikumbusha kuwa ni kinyuma na haki za binadamu kuwaadhibu watu kwa kuwaweka gerezani na kuwatenga na shughuli na familia zao kwa miaka kadhaa mpaka 10, bila ya hatia iliyothibitishwa na Mahakama,” amesema Sheikh Ponda.

 

About The Author

error: Content is protected !!