March 26, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC kutumia mchezo wa Gofu kuchochea ushirikiano wa kibiashara

 

MASHINDANO ya Gofu ya ‘NBC Waitara Trophy 2025’ yamehitimishwa kwa mafanikio makubwa huku mdhamini mkuu wa mashindano hayo, benki ya NBC ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wadau wa mchezo huo ili kuchochea ushirikiano wa kibiashara miongoni mwa wadau, kukuza na kuendeleza vipaji na kutangaza utalii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku moja yakilenga kumuenzi muasisi wake Mkuu wa majeshi Mstaafu, Jenerali George Waitara yaliyohitimishwa na muasisi huyo kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu vya Lugalo Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki yakihusisha washiriki kutoka ndani ya nchi. Wachezaji walionyesha ujuzi, mbinu, na michezo ya kiungwana huku ‘Gofa’ mkongwe Edmund Mndolwa akiibuka mshindi wa jumla wa mashindano hayo.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi mbalimbali wa mashindano hayo, Jenerali Waitara pamoja na kuwapongeza washiriki na wadhamini wa mashindano hayo, aliendeleza wito wake kwa jamii kushiriki kwa wingi kwenye mchezo huo bila kujali dhana ya kuwa mchezo hu oni mahususi kwa watu wa daraja la juu kiuchumi.

“Zaidi niendelee kutoa wito kwa kwa wadhamini wa mashindano mbalimbali ya mchezo huu yakiwemo mashindano haya kuangalia namna ya kupanua udhamini wao mbali na mashindano pekee pia waone namna ya kuboresha viwanja vya mchezo huu hususani kwenye mfumo wa umwagiliaji ili viweze kuwa katika hali nzuri hata kwenye msimu wa ukame,’’ alisisitiza.

Akizungumza kwenye hafla hiyo muwakilishi wa benki ya NBC, Aliko Mwamsaku, Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Muhimbili alisema ushiriki wa benki hiyo kwenye mashindano hayo kwa kiasi kikubwa unasukumwa na adhma ya benki hiyo katika kukuza na kuendeleza sekta ya michezo nchini ili kuibua vipaji, kuchochea ajira kupitia michezo pamoja na kuitumia vema sekta hiyo katika kutangaza utalii wa ndani.

“Pia kwetu mchezo wa gofu tunautazama kama moja ya michezo ya kimkakati inayoweza kuwasaidia wateja wetu kupata wasaa wa kujenga mahusiano ya ukaribu zaidi kupitia michezo na hatimaye mahusiano hayo yakaendelea hadi kwenye biashara zao binafsi na pia zile za taasisi zao kwa kuwa mchezo huu unatoa fursa kwa makundi tofauti ya wana jamii kuweza kukutana bila kujali umri, jinsia au daraja lolote kiuchumi,’’ alisema Mwamsaku.

Akizungumzia ushindi wake, Mndolwa pamoja na kuwashukuru wadhamini wa mashindano hayo benki ya NBC, aliwapongeza wachezaji wenzake kwa ushindani mkubwa waliouonesha. zaidi, Mndolwa aliunga mkono wito wa Muasisi wa mashindano hayo Jenerali Waitara kuhusu uwepo wa mkakati wa makusudi kuhusu uboreshwaji wa uwanja huo hususani kupitia mfumo wa umwagiliaji.

About The Author

error: Content is protected !!