March 18, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wassira amchongea Mo Dewji kwa serikali kwa kutelekeza mashamba ya Rungwe

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira ameitaka serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuangalia uwezekano wa ardhi inayomilikiwa na mwekezaji Mohammed Enterprises Ltd wilayani Rungwe mkoani Mbeya kama imemshinda na haizalishi irejeshwe serikalini ipangiwe matumizi mengine. Anaripoti Mwandishi Wetu, Rungwe, Mbeya … (endelea).

Wassira alitoa kauli hiyo baada ya wananchi wa Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya kudai kuwa Mohammed Enterprises Tanzania Ltd, anamiliki eneo kubwa la mashamba ya chai lakini kwa muda mrefu hajalipwa na hivyo kuwa mapori makubwa yanayoishi nyoka na wanyama waharibifu wakati wananchi hawana maeneo ya kulima.

Hivyo kutokana na kutelekezwa kwa mashamba hayo na kuwa mapori wanaiomba CCM kuielekeza serikali imnyang’anye ili wapate maeneo ya shughuli za kilimo.

Akizungumza wakati akisalimia wananchi wa eneo hilo akiwa katika mwendelezo wa ziara yake mkoani humo, Wasira alisema chama kinaiambia serikali kupitia kwa Waziri wa Kilimo kuwa, ardhi hiyo kama Mohammed Enteprises imemshinda airudishe serikalini halafu serikali itajua namna ya kufanya.

Alisema kwa sababu sheria ya umilikaji wa ardhi inaeleza wazi kuwa ukipewa ardhi ni lazima uzalishe kukuza uchumi kwa kuwa kama mashamba hayo hayazalishi maana yake hata viwanda vya chai navyo haviwezi kuzalisha na matokeo yake uchumi wa wananchi unadidimia.

“CCM hatufanyi kazi ya kudidimza uchumi bali tunao wajibu wa kuhakikisha uchumi wa wananchi unakuwa. Serikali ina sheria inayozungumzia umiliki wa ardhi, kama ni mkulima mkubwa umepewa ardhi ulime maana yake kuna watu wengine hawatakuwa na ardhi hiyo kwa maana umepewa ulime sasa masharti ya kumiliki lazima utekeleze yale uliyokubali. Kama wewe ni mkulima wa chai na umepewa mashamba ya chai ili ukuze uchumi lazima ulime chai, uitunze na uzalishe.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wassira

“Ukiacha kufanya hivyo unavunja mkataba, hakuna mtu anayeruhusiwa kumiliki ardhi, ndiyo maana katika historia yetu tulikataa sheria ya Kingenereza iliyokuwa inaitwa ‘Free Hold’ ambayo ilikuwa inampa mmiliki haki ya kumiliki ardhi hata kama hafanyi chochote na anamiliki milele.

“Hakuna mtu mwenye uwezo kumuondoa lakini sheria hiyo ilifutwa mwaka 1962 ndipo tukaanzisha sheria ya ‘Lease hold’ kwamba wewe ukipewa ardhi haiwi yako, na masharti ya kukodi lazima uwe unafanya kile ambacho umeaihidi kukifanya.

“Sasa kuna Mohamed Enteprises ana ardhi, ana mashamba ya chai hapa Rungwe lakini yameachwa yamekuwa pori. Tunataka kuiambia serikali kutokea Rungwe na kupitia kwa Waziri wa Kilimo, ardhi hii kama Mohammed Enteprises imemshinda na haizalishi airudishe serikalini ili ipangiwe matumizi mengine kwa jinsi itakavyoona inafaa,” alisema.

Aliongeza kwa sababu sheria ya umilikaji wa ardhi ukipewa lazima uzalishe na kimsingi hakuna mgogoro na Mohamed Enterprises ila wana mgogoro wa utekelezaji wa sheria ya uzalishaji, utekekelezaji wa sheria wa kutumia aridhi iliyokodishwa.

Wasira alisema ardhi ya Tanzania ni mali ya wote na Rais amepewa mamlaka ya kuisimamia kwa niaba ya Watanzania, ndio maana kwa anayeshindwa kuiendeleza Rais anayo mamlaka ya kuitwaa.

“Sasa sisi tunamwambia Waziri wa Kilimo maana siwezi kumwagiza Rais, mimi naiagiza serikali kwa maana ya Wizara ya Kilimo ichukue hatua ya kumaliza jambo hili haraka ili tuitumie ardhi ile na itumike kwanza katika mazingira ya Rungwe ambako ardhi ni ndogo.

“Ukiwa nayo wewe ardhi kubwa halafu haitumiki inakuwa dhambi maana watu wengine hawana kwa sababu wewe unayo halafu na wewe huitumii, hiyo sio sawa. Kwa hiyo tunakwenda kufuatilia na kwa kweli nitazungumza na Waziri wa Kilimo kuhusu jambo hili.”

Wakati huo huo, Wasira alisema amepokea pia madai ya wakulima wa chai kutolipwa fedha zao pamoja na wakulima wa kahawa.

“Kwa nini wakulima wa kahawa hawajalipwa? Sababu ninazopewa kuna mgogoro kidogo kati ya ushirika na walipaji na tayari Waziri wa Kilimo amewaita Dodoma ili waende watazame tofauti zilizopo za mauzo na uhusiano wa mnunuzi na chama cha ushirika, lakini jambo hilo lazima limalizwe upesi ili wakulima wa kahawa walipwe fedha zao nalo nitamweleza Waziri wa Kilimo kumuomba alimalize.

“Pia kuna wakulima wa chai wanadai fedha zao na hili halina maelezo wala hakuna mgogoro maana aliyenunua yupo na majani ya chai kwa kawaida huwezi kuyatunza kwani ukiyavuna lazima uyapeleke kiwandani ukiacha yanaharibika.

“Hapa mjue unazungumza na waziri wa zamani wa kilimo, hivyo ninajua mambo haya vizuri sasa kwa sababu hakuna mgogoro tunawaambia kuwa wakulima wa chai hajawalipa kwa miezi miwili. Tunampa wiki mbili Kampuni ya GDM awe ameshawalipa, tena tunamjua na tunayo mawasiliano yake.

“Asipolipa na akileta mchezo tutaiomba serikali siku nyingine imnyime leseni ya kufanyabiashara hiyo kwa sababu hii ni dhuluma na dhuluma ni kitu ambacho CCM hatuwezi kukivumilia, awalipe ndani ya wiki mbili fedha atatoa wapi atajua mwenyewe. Hawa wakulima wanadai sh. milioni 664,” alisema.

Kuhusu malalamiko ya zao la parachichi kutokuwa na soko katika wilaya hiyo, Wasira aliwaeleza wakulima wa zao hilo kuwa wamezungumza kwa hisia kali lakini naye aliuliza kwa nini maparachichi ya Rungwe yawe na matatizo lakini maparachichi ya Njombe hayana tatizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni mtaalamu wa kilimo, Patrick Mwalulenge alitoa sababu za maparachichi ya Rungwe kuwa na bei ya chini ukilinganisha na maeneo mengine na tayari hatua zimechukuliwa kuhakikisha wakulima wananufaika na zao hilo.

“Suala la parachichi nafuatilia kwa karibu sana kuliko mnavyofikiria, wabunge wetu na mimi tulikwenda kwa Waziri wa Kilimo kuzungumzia zao la parachichi. Tulichokubaliana mambo ya muda mfupi na muda mrefu.

“Suala la kwanza sio bei tu bali ni ubora wa parachichi yetu, hata uwe ni wewe unafanyabiashara huwezi kununua bidhaa ambayo ubora wake uko chini. Sasa ubora unapatikana katika maeneo matatu wakati wa kutunza zao lenyewe likiwa hatua ya kutoa maua.

“Parachichi ikiwa hatua ya maua inashambuliwa na ‘fangasi’ wale ‘fangasi’ wanaingia tunda linatengeneza ua usipoweka dawa maana tunda litafungasha lakini hata ukivuna ndani ya siku saba linaharibika.

“Tunda linaoza kwa sababu hewa inaingia sehemu ya kuchumia na hivyo inashambulia tunda lake, hivyo huwezi kupata bei nzuri.

About The Author

error: Content is protected !!