
Dk. Hussein Ali Mwinyi
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema anayodhamira ya kuongeza wanawake katika serikali kwa ngazi zote, hivyo amewahimiza kujitokeza kwa Wingi kugombea nafasi za Uongozi Muda utakapowadia. Anaripoti Apaikunda Mosha. Zanzibar … (endelea).
Rais Mwinyi amesema hayo alipozungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliofanyika Viwanja vya Maonesho Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi Alhamisi ya tarehe 6 Machi, 2025.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa mstari wa Mbele Kuhakikisha Wanawake wanapata fursa Sawa za kiuchumi kupitia Sera na Mipango mbalimbali ya Uwezeshaji,” amesema Mwinyi.
Ameeleza kwamba kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi kiuchumi ZEEA wanufaika 34,746 wamefikiwa na kati yao 17,811 ni Wanawake ambao wamechangia asilimia 51.2 ya wanufaika wote.
Halikadhalika Mwinyi amebainisha kuwa Serikali kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imewezesha utoaji wa Mikopo yenye thamani ya Tsh. 34.9 bilioni ambapo Tsh. 21 bilioni sawa na asilimia 60 zimeelekezwa kwa wanawake.
Amesema dhamira ya kuwezesha wanawake hawa ni kuhakikisha wanashiriki katika uchumi ili kuwapatia fursa ya maendeleao na kumlinda mwanamke dhidi ya utegemezi wa kiuchumi.
Mwinyi amesema ili kuhakikisha hili linafanikiwa tunatakiwa kufanya yafuatayo, kuimarisha majukwaa ya wanawake katika ngazi ya mkoa wilaya, kwa kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa majukwaa hayo kwa kuainisha majukumu ya viongozi katika kila ngazi, kuandaa muongozo wa kuendesha majukwaa ili kuwe na muongozo bora wa kutumia wa kutumia fursa zilizopo ipasavyo.
Mwinyi ameagiza Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Wizara inayoratibu masuala ya Majukwaa kushirikiana na Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Wadau wote Kuandaa Utaratibu wa kuhuwisha Majukwaa ya Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi ili yalete matokeo yaliotarajiwa.
Vilevile amesema muongozo huo unapaswa upewe kipaumbele ili kusaidia kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na kuandaa kanuni za uendeshaji wa majukwaa hayo.
Sambamba na hayo, Mwinyi amezindua rasmi Muongozo wa uanzishwaji wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake Zanzibar pamoja na Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa 2025-2030.
ZINAZOFANANA
Mfumo wa BVR kutumika Uchaguzi Mkuu
ACT Wazalendo kuwashitaki wateule wa Rais Mwinyi
Waziri Mkuu Majaliwa aweka jiwe la msingi bwawa la Kidunda