March 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Muhimbili kuvuna mifupa kwa ajili ya kutengenezea taya ya chini kwa Mil 6.2

Mkurugenzi Huduma ya Upasuaji Muhimbili, Dk. Rachel Mhavile

 

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili imeanzisha huduma ya kuvuna mifupa ya mbavu na nyonga kwa ajili ya kutengeneza taya ya chini ambapo gharama yake ni kiasi cha Sh. 6.2 milioni. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi huduma ya Upasuaji Muhimbili, Dk. Rachel Mhavile wakati wa kutoa taarifa ya mafanikio kwa miaka 4 ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hasani kwa waandishi wa habari katika ukumbi wa Habari Maelezo Jijini Dodoma.

Dk. Rachel amesema kuwa huduma hiyo ni mpya katika hospitali za Umma nchini na itasaidia kuimarisha taya ya chini na mifupa hiyo itavunwa kwa mgonjwa mwenyewe baada ya kufanyiwa vipimo na kuona ni jinsi gani inafaa.

Akitoa ufafanuzi juu ya mifupa hiyo amesema kuwa mifupa itavunwa kwa mgonjwa muhusika anayetaka huduma ya kutibiwa taya na pindi atakapokuwa amepatiwa matibabu hitakuwa moja kwa moja na siyo ya kutoa na kurejesha.

Pia amesema huduma hiyo itasaidia kutengeneza mizizi bandia ya meno ambayo nayo atawekewa mgonjwa na huduma hiyo itapelekea mgonjwa kutokuwa na usumbufu wa kubadilisha mizizi hiyo au taya.

Akizungumzia suala la mafanikio kwa ajili ya watoto wanaozaliwa na tatizo ya kutosikia Dk. Rachel amesema kuwa hospitali imeweza kuanzisha huduma ya upasuaji na kuweka vifaa vya kusaidia kusikia.

Amesema kuwa kwa sasa watoto 54 wamefanyiwa upasuaji na kuwekewa vifaa vya kuwasaidia kusikia kwa gharama ya Sh. 2.3 bilioni kwa wote na kusaidia kuokoa kiasi cha Sh. 4 bilioni kama wangeenda kutibiwa nje ya nchi.

Amesema Hospitali ya Muhimbili imefanikiwa kufanya upandikizaji vifaa vya kusaidia watoto kusikia.

Amesema kuwa Hospitali iliendelea kutoa huduma ya upandikizaji vifaa vya kusaidia kusikia ambapo watoto 54 walihudumiwa na kufanya idadi ya walionufaika kufikia 88 tangu kuanzishwa huduma hii nchini Juni 2017.

Amema Serikali imewagharamia watoto hao 54 kila mmoja ni shilingi milioni 45 sawa na shilingi bilioni 2.43 ambapo kama wangeenda nje ya nchi Serikali ingelipa Sh. 120 milioni kwa kila mtoto sawa Sh. 6.5 bilioni.

Dk. Rachel amesema kuwa kutokana na hali hiyo Tanzania imeokoa kiasi cha kiasi cha Sh. 4 bilioni kama matibabu hayo yangefanyika nje ya nchi na huduma hiyo kupitia hospitali za umma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema huduma hiyo ya upasuaji kwa watoto ni kati ya watoto wa siku moja hadi miaka mitano ambao uchunguzwa na madakitari bingwa na bobezi ambao ni wazawa.

About The Author

error: Content is protected !!