March 4, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Puuzeni propaganda za upinzani uchaguzi utafanyika – Makalla

Amos Makala

 

KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayehusika na Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, amewataka watanzania kupuuza propaganda za upinzani, yaani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba hakuna uchaguzi, aidha kusitisha michango wanayotoa. Anaripoti Apaikunda Mosha, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza siku ya Jumanne ya tarehe 4 Machi 2025, katika kikao cha viongozi wa CCM wa mashina, kata, matawi na mabalozi wa Wilaya ya Kinondoni, Makalla amesema chama hicho kama hakitoshiriki uchaguzi haitakuwa tena chama kikuu cha upinzani baada ya uchaguzi.

Amesema muelekeo wa chama hicho unakwenda kuzima  kabisa matumaini ya wanachama wake waliotegemea kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, amesema kutoshiriki kwa chama hicho kutasababisha  kupotea kwa nafasi zote za uwakilishi ikiwa ni pamoja na wagombea wote (wabunge na madiwani) kukosa nafasi za kugombea.

“Ninawahurumia wanaChadema waliokuwa na ndoto za kugombea ubunge na udiwani na viti maalumu, uongozi huu mpya umefifisha ndoto zao. Chadema kinaenda kuwa chama cha kawaida, si chama kikuu cha upinzani kwa sababu hawatakuwa na madiwani, wabunge wala wagombea urais,” amesema Makalla.

Aidha Makalla amesisitiza kuwa lazima uchaguzi utafanyika kwa sababu chama cha upinzani hakina nguvu wala uwezo wa kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu, pamoja na hayo mabadiliko tayari yalishafanyiwa kazi, hivyo amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.

“Chadema wameshawaambia wafuasi wao wasijiandikishe kwa sababu hakutakuwa na uchaguzi, kwa hiyo wameanza kushindwa kabla, pamoja na mgogoro mkubwa walionao wanajiongezea matatizo kwa kukosa wanachama wao kujiandikisha. Nilimsikia Tundu Lissu akisema ‘Ujiandikishe iweje? So what?’ Nikasema shughuli imeisha hapa, hawa wameshakubali kushindwa, na mimi naomba watanzania wote tukajiandikishe,” amesema Makalla.

Amesema kuwa Chadema wanasema ‘No Reform, No Election’ lakini chama hicho hakina mamlaka wala uwezo wa kuzuia uchaguzi na CCM tayari kimeshafanya hayo mabadiliko na uchaguzi utafanyika, hivo amewataka wananchi kupuuza propaganda kwamba ‘hakuna mabailiko hakuna uchaguzi’ amesisitiza kuwa uchaguzi upo kwa mujibu wa sheria na katiba.

About The Author

error: Content is protected !!