February 25, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

ITC watakiwa kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji nchini

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Mbundi amekitaka Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) kuwekeza katika kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji wa Tanzania ili waweze kuongeza thamani ya bidhaa zao. Anaripoti Apaikunda Mosha. Dodoma … (endelea).

Katika mazungumzo na Meneja Mradi wa Kituo cha Biashara cha Kimataifa, Kelvin Mussa yaliyofanyika Ofisini kwake jijini Dodoma, tarehe 24 Februari, 2025, alitumia fursa hiyo kukishauri Kituo hicho kupanua wigo wa utoaji mafunzo hayo hapa nchini kupitia Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi (VETA) ambavyo vinapatikana kote nchini badala ya kutoa mafunzo kwa wanufaika wachache.

Balozi Mbundi amesema, Tanzania inathamini mchango unaotolewa na Kituo hicho chini ya Program za MARKUP, hata hivyo bado ipo haja kwa Kituo hicho kupanua wigo wa mafunzo kwa wakulima, hususani wa zao la kahawa na wafugaji ili kuwawezesha kuzalisha mazao yao kwa viwango vinavyohitajika lakini pia kuwasaidia kuongeza thamani ya mazao hayo badala ya kuuzwa kama malighafi.

Akizungumzia biashara ya ngozi, Balozi Mbundi amesema kuwa Tanzania bado haijanufaika kikamilifu na mazao yanayotokana na mifugo ikiwemo Ngozi licha ya kuwa ni nchi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika baada ya Ethiopia na Sudan Kusini.

“Katika hili naomba muangalie namna ambavyo Tanzania pia itanufaika na uwepo wa Taasisi ya Ngozi ya Afrika kama ilivyo kwa nchi nyingine zenye idadi kubwa ya mifugo barani Afrika,” alisisitiza Balozi Mbundi.

Aidha, Balozi Mbundi amesema upo umuhimu wa kuwajengea uwezo wakulima katika sekta ya ubunifu, uwekaji alama na vifungashio ili kuwezesha bidhaa za kahawa zinazozalishwa hapa nchini kupenya kwa urahisi katika masoko ya kiamataifa hususani yale ya Ulaya.

About The Author

error: Content is protected !!