February 24, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Makamba amhakikishia Rais Samia kushinda kwa kishindo Lushoto

 

MBUNGE  wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba, amesema atahakikisha anaongeza motisha kwa wananchi kuendelea kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu ameleta miradi ya maendeleo ambayo imesaidia kuongeza ubora wa maisha ya watu. Anaripoti Apaikunda Mosha, Lushoto, Tanga … (endelea).

Akizungumza leo 24 Februari 2025, katika mkutano wa hadhara wilayani Lushoto, ameeleza kuhusu historia ya matokeo ya uchaguzi wa Rais, amesema kuwa tangu mwaka 1995, kura za urais kwa mgombea wa CCM zimekuwa juu na hivyo ataendelea kushikilia na kuhakikisha kuwa Bumbuli haishuki chini ya asilimia 90 kwa kura za CCM.

Amesema namna ambavyo serikali imewakumbuka Bumbuli kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na barabara ambazo zilikuwa ni changamoto kubwa na ya muda mrefu, hatua ambayo itarahisisha usafiri na kukuza uchumi wa eneo hilo.

“Kwa miaka mingi, barabara zetu zilikuwa ni changamoto kubwa kwetu. Lakini juzi, takribani wiki tatu zilizopita, tumepokea taarifa kuwa barabara hizi zitajengwa kwa kiwango cha lami. Hii ni habari njema kwa wananchi wa Bumbuli na kwa wananchi wa Lushoto kwa ujumla. Utakuwa umeacha historia kubwa sana katika milima hii ya Usambara,” alisema Makamba.

Aidha, Makamba alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kumteua kushika nafasi ya Waziri wa Nishati na baadaye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amesema ni heshima kubwa sana kwake hata hivyo amemjengea uwezo  katika utumishi wake, alama ambayo atabaki nayo maishani mwake.

About The Author

error: Content is protected !!